Home » » PROFESA MAGHEMBE ATEMBELEA BOMBA JIPYA LA RUVU CHINI

PROFESA MAGHEMBE ATEMBELEA BOMBA JIPYA LA RUVU CHINI

Written By JAK on Tuesday, January 14, 2014 | 5:56 AM


Na Athumani Shariff

WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ametembelea mradi wa ulazaji wa bomba jipya la maji kwenye mradi mkubwa wa maji kutoka Ruvu chini, Mji mdogo wa Bagamoyo, utakao leta maji zaidi ya lita milioni 270 kwa siku.

Mradi huo uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 54 unakabiliwa na changamoto kubwa mbili zikiwemo za uhaba wa umeme katika kiwanda cha kutengeneza mabomba jambo ambalo linakwamisha upatikanaji wa mabomba yaliyyokadiriwa na kampuni hiyo ya Sinohydro inayotekeleza mradi huo.

Changamoto nyingine iliyoelezwa katika mradi huo ni kesi zilizofunguliwa dhidi ya Mamlaka ya Maji Safi Dar es Salaam (DAWASA), kesi 12 zipo mahakani ambazo mamlaka hiyo imepanga kuzishughulikia haraka iwezekanavyo.

Akijibu swali la waandishi wa habari juu ya hatua zinazochukuliwa na DAWASA katika kukabiliana na kesi hizo, Mwenyekiti wa bodi ya DAWASA Bi. Hawa Sinare alisema mpango uliopo ni kuonana na Jaji Mkuu kusaidia kesi hizo zisikilizwe kwa haraka na zitolewe hukumu mapema ili zisikwamishe mradi huo mkubwa wenye manufaa kwa watu walio wengi.

Profesa Maghembe pia alitembelea upanuzi wa mtambo wa kusukuma maji uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 98 wa Ruvu Chini Mji mdogo wa Bagamoyo uliojengwa ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa jiji la Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo.

Awali Mtambo wa maji wa Ruvu chini kabla ya upanuzi ulikuwa ukizalisha lita za ujazo milioni 180 kwa siku, wakati huu wa sasa utaongeza lita za ujazo miliono 90 na kufanya lita za ujazo milioni 270 kwa siku kupelekwa jijini Dar es Salaam.

Kuongezeka kwa lita hizo za ujazo katika uzalishaji kunatarajiwa kupunguza ukosefu wa maji kwa wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha na Bagamoyo ambao watapata maji kwa matumizi ya majumbani na viwandani.

Waziri wa Maji pia aliongeza kuwa kazi ya upanuzi pia itaendelea katika mtambo wa Ruvu juu baada ya kukamilika mradi wa Ruvu chini na tayari pesa zake zipo zimeshatengwa zaidi ya bilioni 130. Aidha alisema, pia uchimbaji wa visima na mabwawa utaongeza upatikanaji wa maji na shida ya maji kuwa historia jijini Dar es Salaam.

Akijibu swali juu ya kadhia ya maji jijini Dar es Salaam, Profesa Maghembe alisema, miradi ya maji haihitaji siasa, na wala huwezi ukaijenga kwa siku moja, nafikiri munaona ujenzi wake, huu mradi ni mkubwa na unahitaji utaalamu wa hali ya juu na hata kasi yake ya ujenzi munaiona.

“Niwaambie wakazi wa Dar es Salaam nafahamu tabu wanayoipata kuhusu uhaba wa maji na kwakulijua hilo ndiyo maana natafuta suluhisho lakudumu, na maji haya kwa miradi hii yote itakuwa na uwezo wa kulihudumia jiji la Dar es Salaam mpaka mwaka 2034 bila shida ya maji na pia miundombinu ya kuongeza upatikanaji wa maji baada ya mwaka 2034 pia ilishawekwa” aliongeza Waziri Maghembe.
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe wa mbele akiwa amesimama juu ya bomba jipya Boko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Ulazaji wa bomba hilo umekamilika kwa asilimia 54. Nyuma yake ni maafisa wa Wizara ya Maji, Dawasa na wahandisi wa mradi.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe wa kwanza kulia, akipewa maelezo juu ya pampu za kusukumia maji. Pampu moja inauwezo wa kusukuma lita milioni 90 kwa siku. Na huwa sinasukuma pampu tatu na moja hubaki akiba endapo moja itaharibika ili kufanya maji kusukumwa kwa ujazo uliokusudiwa.


Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger