Home » » Upande wa Pili wa Operesheni Tokomeza

Upande wa Pili wa Operesheni Tokomeza

Written By JAK on Friday, January 3, 2014 | 6:06 PM

Hisia hazisikii sauti ya mantiki 

http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2116690/highRes/647144/-/maxw/600/-/juqrph/-/kagasheki.jpg

KUNA tofauti kati ya maneno KWELI na U-KWELI, ingawa maneno haya yanatumika mara nyingi kuelezea jambo moja. Neno kweli linaweza kuwa na ukweli zaidi ya mara moja. Kila mtu anaweza kuwa na ukweli wake juu ya kweli moja.

Kilicho kweli ni kuwa Operesheni Tokomeza iliendeshwa, lakini kuna ukweli zaidi ya mmoja, ule tuliousikia kutoka kwenye Kamati ya Bunge na ule mwingine ambao haujapata nafasi ya kusemwa au kwa mazingira yalivyo, hausemeki na haupokeleki.

Niweke wazi, naunga mkono Operesheni Tokomeza na nasikitika kwa matatizo yaliyojitokeza ambayo ni ajali ya kioperesheni. Ajali ya kioperesheni kama ilivyo ajali ya kikazi inaweza kutokana na uzembe au hitilafu ya kitendea kazi/mfumo.

Bahati mbaya suala la Operesheni Tokomeza liliingia hisia na hivyo limezaa hisia. Hata mjadala wake umejaa hisia kiasi kwamba ukijadili kinyume chake unaonekana wa ajabu. Hata Profesa nguli kama Issa Shivji naye (katika makala yake toleo la gazeti hili lililopita) alijadili kwa hisia.

Kamati ya Bunge nayo walimezwa na hisia na haishangazi waliwasilisha ripoti ile mbele ya Bunge kwa hisia, wabunge wote wakajadili ripoti hiyo kwa hisia kubwa. Mara nyingi ni vigumu kushindana na hisia, kwa sababu hisia hazisikii sauti ya mantiki.

Hakuna namna, serikali ingejitetea, ingefafanua na ikaeleweka, hisia zilikuwa lazima zishinde. Upepo utakapotulia na hisia zikashuka, mantiki itajitokeza.

Operesheni Tokomeza inatajwa kuendeshwa kwa namna ambayo imedhalilisha utu na kuminya haki za binadamu. Operesheni hiyo pia imesababisha mauaji ya 'raia' 13. Neno raia nimeliweka katika kifungua na kifunga usemi kwa kuwa linapaswa kutumika kwa tahadhari kubwa. Hali kadhalika, askari sita nao wamefariki katika Operesheni Tokomeza, hawa hawatajwi wala hawatamkwi, hawaonekani kama nao ni binadamu, wala hawajadiliwi wameuawa na nani. Kupoteza raia ni jambo kubwa, kupoteza askari ni jambo kubwa zaidi. Si rahisi kwa askari kufa katika operesheni dhidi ya raia, isipokuwa tu kama 'raia' nao wanapambana.

Dhana potofu kuhusu Operesheni Tokomeza

Kuna maneno mawili ambayo yanatumika bila tahadhari katika suala hili. Neno la kwanza ni 'operesheni' na neno la pili ni 'raia'. Kwanza, operesheni ni mapambano dhidi ya hatari fulani. Operesheni ni 'ama zao-ama zetu' na kawaida huambatana na athari (damages) kwa kuwa inaendeshwa dhidi ya kikundi au adui ambaye naye ana nguvu.

Kutangaza operesheni maana yake ni kuwa hatari iliyopo haiwezi kudhibitiwa kwa mbinu na medani za kawaida za ulinzi na usalama. Isitoshe, aina ya silaha na kikosi, inategemea sana na aina ya tishio na makisio ya uwezo wa adui mwenyewe.

Kinachofanya operesheni kuitwa ya mafanikio, ni pale inapofikia lengo na inapokuwa na athari ndogo ikilinganishwa na lengo lililofikiwa. Kwa kifupi, mafanikio ya operesheni hayamaanishi kuwa hakuna madhara, bali madhara ni madogo kuliko faida.

Neno la pili ambalo linatumiwa vibaya ni 'raia'. Dhana inayojengwa hapa ni kuwa raia wote ni wema wakati wote, na kuwa majangili si raia. Kwa haraka haraka, tunaaminishwa kuwa Operesheni Tokomeza ililenga majangili na si raia ambao ni majangili. Majangili hawa wamejitenga mbali na raia, wanaishi mahala fulani wamekusanyika ambako vikosi vya operesheni vilitakiwa vikawakute huko na kupambana nao, na si kuwatafuta miongoni mwa raia.

Tunachojisahaulisha ni kuwa, taarifa za kukamatwa kwa meno ya tembo zimeonyesha majangili hawa wakikamatiwa majumbani kwa raia wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara, wanasiasa, wanawake, wanaume na hata watumishi wa umma na vyombo vya dola. Kwa mlinganyo huu, ni vigumu kutenganisha raia mwema na jangili, pia inakuwa vigumu wigo wa mapambano kuishia porini pekee bila kuendesha operesheni uraiani.

Mantiki na haja ya operesheni

Ilipotangazwa Operesheni Tokomeza wabunge, wananchi na wadau wa uhifadhi na mazingira walifurahia.

Walifurahi kwa kuwa wote waliguswa na kasi ya kutisha ya ujangili uliokuwa ukiendelea nchini. Inakadiriwa kuwa Tanzania imepoteza nusu ya idadi ya tembo wake katika kipindi cha muongo mmoja. Taarifa za kukamatwa shehena mbalimbali za meno ya tembo zilikuwa zimezizima na mbaya zaidi zikihusisha hata askari wasio waaminifu kukamatwa na meno hayo wakitumia magari ya serikali.

Kulikuwa na kilio kote nchini cha kulaumu serikali kwa kutochukua hatua. Tena, ikumbukwe kuwa umma ulitaka serikali kuchukua hatua kali, ndio maana haishangazi kuwa umma ulifurahia habari za kuanzishwa kwa Operesheni Tokomeza bila hata kutaka kujua itaendeshwaje. Walichoshwa na ujangili kuliko kujali madhara yatakayotokana na operesheni. Pengine kutokana na kugubikwa na hisia, hawakufikiria ama walisahau kuwa operesheni ni mapambano na sio lelemama.

Shinikizo kubwa lilikuwepo kutoka nje ya nchi. Jumuiya ya Kimataifa ilitaka kuona Tanzania ikichukua hatua.

Suala hili la ujangili lilizungumzwa na Rais Barack Obama alipokuja nchini. Mikutano kadhaa iliitishwa duniani wakitaka kuona Jumuiya ya Kimataifa ikiungana kudhibiti ujangili. Ilishtua zaidi, pale ilipogundulika kuwa, mtandao huu wa ujangili ni wa kimataifa na unahitaji ushirikiano wa kimataifa kukabiliana nao. Jumuiya ya Kimataifa nayo ilipokea kwa furaha taarifa za Tanzania kuanzisha Operesheni Tokomeza ujangili. Kwa ufupi, wakati ulikuwa muafaka na lengo lilikuwa muafaka. Hapakuwa na mbadala zaidi ya serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza.

Maandalizi na utekelezaji wa Operesheni

Kimsingi, kunakodaiwa kufeli kwa Operesheni Tokomeza kunaonekana katika maandalizi na utekelezaji wa operesheni na si mantiki ya kuanzishwa kwake. Nikiri awali kuwa taarifa za maandalizi na utekelezaji wa operesheni ni taarifa za siri ambazo haziko wazi kwa umma. Hata Kamati ya Bunge imekiri kuwa mchakato mzima ulikuwa ukiendeshwa kwa usiri. Ukweli huu, hautuzuii kung'amua matatizo yanayoweza kuchangia kunakoitwa kufeli kwa operesheni hii madhali sasa taarifa za kutosha za operesheni hiyo zimetoka nje.

Kinachoonekana haraka haraka ni kuwa inawezekana kuwa kulifanyika makosa katika ukusanyaji wa taarifa za uchunguzi wa nani hasa wanahusika na mtandao huo.

Haifahamiki vizuri ni kwa kiasi gani kamati za usalama za wilaya na mikoa zilihusishwa, na pale zilipohusishwa zilichangia kwa kiasi gani katika umakini wa taarifa zao za uchunguzi. Taarifa za kamati hizi za usalama za wilaya na mikoa ni muhimu kwa kuwa huko ndiko ujangili unakotendeka. Hata hivyo, changamoto kubwa ni kuwa, kamati hizi pengine hazikuwa za msaada sana kwa kuwa wajumbe wa kamati hizi, baadhi ni washiriki au wafaidikaji wa mtandao wa ujangili.

Tatizo jingine kubwa linaloweza kuchangia upungufu wa Operesheni Tokomeza ni operesheni zingine zilizokuwa zikiendelea dhidi ya wafugaji. Itakumbukwa katika Bunge la Oktoba, 2013 kuliibuka mjadala mkali kutoka kwa wabunge wanaowakilisha maeneo ya wafugaji juu ya wafugaji kuonewa kwa kuzuiliwa malisho ya mifugo yao.

Tayari uhusiano kati ya wafugaji na wakulima ulikuwa umekwishasababisha maafa na chuki za kijamii. Serikali za vijiji, wilaya na mikoa nazo zilikuwa lawamani kwa kushindwa kudhibiti migogoro hii, na wakati mwingine zikituhumiwa kutoa upendeleo, hasa kwa wakulima kutegemeana na wapi serikali hizo zipo, kwa maana ya maeneo ya wakulima wengi au wafugaji wengi.

Hivyo, haitii shaka kuwa, baadhi ya watendaji wa ngazi za vijiji, wilaya na mikoa waliiona Operesheni Tokomeza kama mwanya wa kutokomeza tatizo la wafugaji wa kuhamahama, waliopachikwa jina la 'wafugaji haramu'. Ndio maana, tunakuta katika Operesheni Tokomeza Ujangili wanauwawa wafugaji na mifugo.

Kuna uwezekano kuwa baadhi ya sehemu taarifa zilipotoshwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya kutokana na wajumbe kuwahisi tu baadhi ya watu kuwa ni majangili au wanahusika nao. Matatizo kama haya yalijitokeza pia wakati wa operesheni dhidi ya biashara ya viungo vya albino. Pengine, uharaka wa kufanikisha operesheni hiyo ulitokana na shinikizo la ndani na nje ya nchi bila kutoa muda wa kutosha wa maandalizi. Hali kadhalika, matatizo haya inawezekana yametokana na udhaifu wa kiuratibu kwa vile operesheni ilihusisha wizara tatu.

Pengine, upungufu ama udhaifu huo, uliwalazimu waendesha operesheni kutumia mbinu ya kutesa ili kukusanya taarifa zaidi. Kwa ufupi, mbinu hii ya utesaji ni kielelezo cha kukosekana kwa weledi katika maandalizi na ukusanyaji wa taarifa.

Kwa kiasi kikubwa, ufanisi wa operesheni unategemea ukamilifu wa maandalizi ya mezani kabla ya kufika uwanjani. Kwa maelezo yoyote yale, kama operesheni inasemwa kuwa imefeli, basi kufeli huko lazima kutokane na upungufu katika maandalizi na utekelezaji.

Operesheni kusitishwa kabla kukamilishwa

Tutakumbuka kuwa Operesheni Tokomeza ilisitishwa mapema tu baada ya kuanza kwake. Kusitishwa huko kulitokana na vilio vya wabunge na kulizaa Azimio la Bunge la kuunda kamati ndogo ya Bunge, kuchunguza na kutoa taarifa na mapendekezo bungeni.

Wakati operesheni hiyo inasitishwa, takwimu zilionyesha kuwa askari sita na raia 13 waliuawa na kulikuwepo kesi 687 na watuhumiwa 1,030 na meno ya tembo 706 yalikamatwa, ambayo ni sawa na tembo 353 waliouawa. Takwimu hizi ni vyema zikazingatia kuwa operesheni hii imedumu kwa siku zisizozidi 28, yaani kuanzia Oktoba 5  hadi Novemba mosi, 2013.

Binafsi napata taabu sana kusema kuwa Operesheni Tokomeza imefeli. Napata taabu zaidi kuelewa vigezo vinavyotumiwa na wale wanaosema operesheni imefeli. Ni vigumu kusema operesheni imefeli wakati haikumalizika baada ya kusitishwa katikati.

Pia, takwimu za idadi ya watuhumiwa, kesi na meno ya tembo yaliyokamatwa kwa kipindi hicho, hayashawishi kusema kuwa operesheni imefeli. Isitoshe, katika kipindi hicho, hata baada ya operesheni kusitishwa, taarifa za matukio ya ujangili hazisikiki au zimepungua sana. Ni vigumu kubisha kuwa operesheni hii imeshitua majangili ama ilisambaratisha mtandao wao kwa kiasi kikubwa.

Tayari, ziko sauti zinazotahadharisha kuwa kusitishwa huku kwa operesheni kunatoa mwanya kwa majangili kujipanga upya, pia zipo sauti za kusema operesheni iendelee isipokuwa isimamiwe vizuri zaidi.

Binadamu ni viumbe wa hisia. Hisia moja hufunika nyingine. Hisia zilizoamshwa na vifo na madhila yaliyowafika baadhi ya raia ambao hatujui kama walikuwa ni raia wema, majangili au washirika wa majangili zimegubika faida na matokeo yote chanya ya operesheni hii. Operesheni yote imeonekana mbaya na ya kikatili. Historia inatufundisha kuwa hata katika Operesheni Vijiji vya Ujamaa, kulikuwepo malalamiko makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu ingawa unaweza usifikie huu wa sasa. Leo, tunaishi matunda ya Operesheni Vijiji vya Ujamaa, tunajenga shule, zahanati kila kijiji na sasa tunapeleka umeme vijijini kwa kuwa vijiji vipo.

Msingi wa hoja hapa ni kuwa, Operesheni Tokomeza haikufeli kabisa. Ni vigumu kusema pia ilikuwa na mafanikio makubwa na mazuri. Kama nilivyosema awali, mafanikio makubwa ya operesheni yoyote ni pale ambapo imeendeshwa kwa ufanisi kiasi cha kutokuwa au kuwa na madhara madogo yasiyotarajiwa.

Operesheni Tokomeza haikupewa muda wa kutekeleza vya kutosha kiasi cha kuweza kupima uwiano kati ya matokeo na madhara, pengine mwishowe pangelikuwepo na mafanikio makubwa sana kuliko madhara.

Hali kadhalika, mtu mwingine angeweza kusema kuwa operesheni hii ingeendelea madhara yake yangezidi mafanikio. Majumuisho yote haya yana mantiki kwa kuwa operesheni ilisitishwa njiani. Tunachoweza kusema ni kuwa Operesheni Tokomezo ilikuwa na mseto wa mafanikio, madhara na mafunzo mengi kwa taifa letu.

Hatua za uwajibikaji

Uwajibikaji hauepukiki katika Operesheni Tokomeza hata kama ingekuwa ya mafanikio. Operesheni hii kwa asili ilikuwa iambatane na gharama za kisiasa. Operesheni Tokomeza haikuwa operesheni ya kawaida, kiwango cha tishio na hatari iliyoletwa na ujangili kuliifanya operesheni hii kuwa ya kufa au kupona. Adui hakuwa wazi maana hakuna jeshi la majangili, adui huyo amejificha miongoni mwa raia tena wakati mwingine katika kivuli cha mwanasiasa, mtendaji, mfanyabiashara na hata mwanamke. Ilikuwa vigumu kwa hali yoyote kuepuka kudhuru raia mwema, ambacho kingewezekana tu ni kudhibiti madhara hayo kuwa madogo sana kwa kutumia mbinu za kisayansi, kiintelijensia na medani za juu za kivita.

Napata taabu kukubaliana na wale wanaosema kuwa serikali isingetumia jeshi au kutobughudhi raia. Katika washiriki 2,371, wanajeshi walikuwa 885 au asilimia 37. Polisi walikuwa 480 au asilimia 20 tu. Napata taabu kwa kuwa, tayari kikosi cha wanyamapori kilishaelemewa na majangili. Takwimu zinaonyesha kuwa, askari wanyamapori 1,000 wamepoteza maisha Afrika mwaka jana, wakipambana na ujangili kwa kuwa majangili hawa wana mafunzo ya kijeshi na wanatumia silaha nzito.

Aidha, hatuna polisi wa kutosha wa kujazia asilimia 37 ya nguvu kazi ya wanajeshi walioshiriki Operesheni Tokomeza bila kuathiri uwezo wa Jeshi la Polisi kuendelea na majukumu yake ya kila siku ya usalama wa raia na mali zao. Ikumbukwe kuwa Jeshi la Polisi tayari lina lawama nyingi ikiwa ni pamoja na askari wachache ukilinganisha na mahitaji makubwa ya nchi. Sioni njia nyingine ambayo serikali ingetumia zaidi ya kutumia sehemu ya jeshi, kinyume cha kufanya hivyo, ingelazimu serikali kukodisha polisi nje ya nchi, jambo ambalo kiusalama halileti mantiki. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina wajibu na jukumu la kulinda nchi wakati wa vita na wakati wa amani.

Taharuki iliyoikumba serikali inaweza kuelezewa vyema na simulizi ya Jenerali Wojciech Jaruzelski, Mtawala wa Poland aliyoitoa mwaka 1981 akiwa ughaibuni akilaumiwa kwa mauaji makubwa yaliyotokea baada ya yeye kutangaza hali ya hatari iliyosababisha wanajeshi kuingia mtaani kudhibiti usalama.

Alipoulizwa na mwandishi baadaye, baada ya kustaafu ni kwa nini alitoa uamuzi wa hali ya hatari uliosababisha maafa makubwa, alijibu ifuatavyo: "Nimeshahukumiwa na magazeti, lakini napenda kuwakumbusha wanahistoria uchwara kuwa, si mimi niliyeumba mazingira ya historia yaliyokuwapo.

Historia ilinifikisha katika hali ambayo sikuwa na jinsi zaidi ya kuchagua baina ya machaguo mabaya mawili (sio chaguo moja baya na jingine zuri). Uchaguzi wowote ambao ningeufanya ungekuwa na matokeo mabaya, nilikuwa katika wakati mgumu, mimi ni mzalendo siwezi kuitwa muuaji, kwa kuchukua uamuzi ule wa kutangaza hali ya hatari, niliiokoa Poland kutoka kwenye hatari kubwa zaidi".

Mazingira aliyofanyia uamuzi Jenerali Jaruzelski yanafanana na mazingira ambayo serikali ilifikishwa katika kuamua kuanzisha Operesheni Tokomeza. Serikali ilikuwa na machaguo mawili tu nayo yote yalikuwa yaishie kwenye kulaumiwa.

Ilikuwa ni aidha uache tembo watokomee ulaumiwe, au upambane na ujangili ulaumiwe. Kupambana na ujangili ilikuwa ndio chaguo lenye afadhali kati ya machaguo hayo mawili. Hatimaye, serikali ingeishia kuwajibika.

Nawapongeza mawaziri waliowajibika kwa niaba ya serikali, nampongeza zaidi Rais Jakaya Kikwete kwa kuwakubalia kufanya hivyo. Angeliweza kukataa na anayo mamlaka ya kufanya hivyo. Serikali ingeweza kutaka kujitetea juu ya kilichotokea na pengine ingeilazimu serikali kutoa taarifa za kiusalama ambazo si busara zitolewe hadharani.

Kuwajibika kwa serikali kuna maana ya kukiri udhaifu na madhara yaliyojitokeza, kuelezea masikitiko yake kwa wale walioathirika, kujifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza na kurejesha imani kwa wananchi juu ya serikali.

Tunaelekea wapi baada ya hapa?

Serikali pamoja na mambo mengine imechaguliwa iongoze, iamue na itekeleze. Serikali haiwezi kukwepa kulaumiwa katika kutekeleza wajibu huo. Mamlaka ya juu kabisa katika nchi yenye dhamana juu ya watu, uhai na mali zao ni serikali, hivyo lazima ilaumiwe pale uhai na mali za watu zinapopotea aidha kutokana na serikali kutotenda au kutenda. Serikali ililaumiwa kwa kutopambana na ujangili na mtandao wake unaowahusisha wafanyabiashara na wanasiasa, hali kadhalika imelaumiwa kwa kupambana na mtandao huo.

Operesheni Tokomeza imetufundisha mengi tuliyoyajua na ambayo hatukuyajua. Kama nilivyosema, operesheni hii haikuepukika, na labda ilipaswa kutokea ili kutushitua kuhusu udhaifu wa kimfumo na kimuundo uliokuwapo.

 Pengine, pasingekuwapo na Operesheni Tokomeza, tungekuja siku moja kugutushwa na janga kubwa zaidi.

Wachina wana msemo wao kuwa "kila janga huja na fursa zake". Ni wakati sasa wa kuangalia fursa zitokanazo na majanga yaliyotokana na operesheni hii. Operesheni Tokomeza inatupa mafunzo kadhaa.

Mosi, operesheni si njia nzuri ya kutatua matatizo na yatupasa sasa kujenga tabia ya kuyakabili matatizo yakiwa bado madogo kabla hayajaota mizizi na kuhitaji operesheni. Hivi sasa liko janga la dawa za kulevya, na hili la wafugaji na wakulima. Hali inavyokwenda kama hayatadhibitiwa, itatulazimu operesheni siku za usoni na serikali italazimika kuwajibika.

Pili, Operesheni Tokomeza imetufundisha udhaifu mkubwa ulioko katika mifumo ya serikali ngazi za wilaya na mikoa, hususan kamati za usalama. Huko nako kunahitaji kusukwa upya na kuimarisha mfumo wa utawala. Laiti wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wabunge wangefanya kazi vizuri, tusingefikishwa hapa.

Tumefikishwa katika operesheni kwa kuwa ngazi za wilaya na mikoa zilielemewa ikalazimu kunusuriwa kitaifa, yaani operesheni. Migogoro ya wakulima na wafugaji na ulinzi na usalama wilayani na mikoani unahitaji uratibu na uongozi kwanza, silaha baadaye.

Tatu, Operesheni Tokomeza inatuamsha kufanya tathmini na kuboresha uwezo wa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama. Uhalifu unapanuka duniani kote na unajiimarisha kiteknolojia, kiintelijensia na kimtandao. Majeshi yetu nayo yanapaswa kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko haya. Tunahitaji kuongeza uwezo wao wa kufanya operesheni za ndani ya nchi, na muhimu ushirikiano kati ya majeshi ya ulinzi na usalama katika kutekeleza majukumu yao. Ni vyema tukawekeza katika kuyawezesha majeshi yetu nchini kufanya mazoezi na mafunzo ya pamoja hususan katika kukabili majanga. Muhimu zaidi, kuyaelimisha zaidi juu ya wajibu wao kwa raia na kurejesha imani yao kwa wananchi ambayo imeporomoka sana.

Nne, operesheni tokomeza inakumbusha serikali juu ya kuhimiza wajibu wa wananchi katika ulinzi wa nchi yao. Serikali imeacha kuhimiza na kuelimisha umma juu ya wajibu huu. Pale wananchi wanapowajibika katika ulinzi na usalama wa nchi, wahalifu wakiwemo majangili hawawezi kutufikisha hatua ya operesheni.

Sote tunafahamu, majangili hawaishi porini, wanaishi miongoni mwetu, tunakula nao, tunakunywa nao na kuishi nao. Wananchi wanapaswa kuwafichua na kushirikiana na dola kuwatokomeza. Kinyume cha hapo, majangili na wahalifu watawaponza raia wema pale operesheni itakapopita, maana itawia vigumu kutofautisha raia na jangili.

Aliwahi kusema Wiston Churchil, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kuwa, "Mataifa na watu wake hupata busara baada ya kumaliza fursa zote". Tukijenga utamaduni wa kutumia fursa za kurekebisha maovu mapema, hatutalazimika kuja kung'amua busara baada ya kuwa tumedhurika, kama ilivyotokea kwa Operesheni Tokomeza.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger