Na Hassan Simba, Mtwara
IMEELEZWA kuwa kufikishwa kwa elimu juu ya mpango wa kunusuru kaya masikini unaoendeshwa na mfuko wa maendeleo ya jamii nchini tasaf awamu ya tatu, ndio chachu ya mafanikio ya mpango huo yaliyokwishaanza kuonekana kwa jamii ya wakazi wa Mtwara.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa mfuko huo Bw. Ladislaus Mwamanga, alipokuwa anaongea na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Idd Mshili, ofini kwake alikokwenda kumtembelea kabla ya kwenda vijijini kujionea namna mpango huo unavyotekelezwa wilayani humo.
Bw. Mwamanga alisema kuwa chini ya mpango huo wawezeshaji wamelimishwa vizuri na wao wanaweza kufikisha ujumbe kwa jamii na baada ya kuanza kuelewa ndio maana kumekuwa na mwitikio chanya katika maeneo yote ambako mradi huo umeanza kutekelezwa.
"Ndugu mkurugenzi hayo mafanikio unayoanza kuyaona hata kabla ya kuanza kutolewa kwa ruzuku kwa kaya masikini ni matokeo ya elimu ambayo tumewapatia jamii...kwa hakika tumepata mwitikio mzuri kila tulikoenda na hii inatutia faraja na kutuongezea hali ya kufanyakazi kwa bidii", alisema Mwamanga.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo baada ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kuueleza ujumbe wa tasaf makao makuu uliomuhusisha mwakilishi kutoka benki ya dunia.Idda Manjolo. kwamba tayari mafanikio ya mpango huo yameshaanza kuonekana katika wilaya yake hata kabla ya ruzuku kuanza kutolewa kwa kaya masikini.
"Nataka niwaambie tu kwamba wakati nyinyi mnasema mpango huu upo katika hatua ya pili ambayo ni kutambua kaya masikini na hatua ya tatu ndio itakuwa ya kuanza kutoa ruzuku lakini hapa kwetu tumeanza kuona mafanikio...uandikishaji wa watoto wa darasa la kwanza umevuka lengo na wakinamama wanaohudhuria kliniki imeongezeka mara dufu", alisema Mshili.
Mshili alisema kuwa kwakua mpango huo unalenga pia kutoa ruzuku kwa kaya masikini ambazo watoto wao wanahudhuria shuleni kaya nyingi zimehamasika kuandikisha watoto wao na kufuatilia mahudhurio yao ili kuweza kupata sifa ya kupata ruzuku hiyo na hjivyo kufanya maeneo mengi kuvuka malengo ya uandikishaji waliyojiwekea.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa ya mafanikio kwani katika kipindi cha nyuma wataalamu wake wamekuwa wakiwahimiza wananchi kuwapeleka watoto wao shuleni na wakinamama kuhudhuria kliniki lakini mwitikio ulikua mdogo kulinganisha na baada ya kuanza kwa mpango huo wa tasaf.
Akiwa katika kijiji cha Chawi alikukonda kuona namna ambavyo wanakijijikupitia mkutano wao mkuu wa kijiji wanachaguana kuongoza kamati ufuatiliaji na kuthibitisha majina ya kaya masikini, mkurugenzi huyo alisifu uwazi katika uendeshaji wa zoezi na uelewa mkubwa wa wawezeshaji juu yanmpango huo.
Mwamanga alisema chini ya mpango huo uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete 2012 na kuanza kwa majaribio katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Chamwino, kaya masikini zinapatiwa ruzuku katika elimu, afya na kujikimu kimaisha kila mwezi kwa miaka mitatu ambapo hadi sasa halmashauri 22 zimekwishafikiwa.
Mwamanga alisema kwa namna walivyojipanga hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu halimashauri zote kwa upande wa Tanzania bara na visiwani zitakuwa zimefikiwa na mpango huo ambao unalenga kupunguza umasikini miongoni mwa jamii nchini.
Mwezeshaji wa jamii wilaya ya Mtwara, Yusufu
namoto, akisoma majini ya kaya masikini zitakazoingia katika mpango wa kunusuru
kaya masikini katika mkutano wa kijiji cha Chawi wilayani humo ambapo ujumbe wa
tasaf makao makuu ukiongozwa na mkurugenzi mtendaji. Ladislaus Mwamanga,
mwakilishi wa benki ya dunia Ida manjolo.
Wananchi katika mkutano wa kijiji cha Chawi
Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa maendeleo ya
jamii nchini (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga, (mwenye suti nyeusi) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa serikali ya kijiji cha Chawi wilaya ya Mtwara mkoani hapa
mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kijiji uliothibitisha majina ya kaya
masikini zitakazoingia katika mpango wa kunusuru kaya masikini, kushoto kwake
ni mwakilishi wa benki ya dunia Ida Manjolo
Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa maendeleo ya
jamii nchini. Ladislaus Mwamanga, (mwenye suti nyeusi) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe wa serikali ya kijiji cha Chawi wilaya ya Mtwara mkoani hapa
mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kijiji uliothibitisha majina ya kaya
masikini zitakazoingia katika mpango wa kunusuru kaya masikini, kushoto kwake
ni mwakilishi wa benki ya dunia Ida Manjolo
Post a Comment