Home » » CHADEMA sasa wazozana wao kwa wao

CHADEMA sasa wazozana wao kwa wao

Written By JAK on Thursday, March 13, 2014 | 10:13 PM


Source: Paul Sarwatt Arusha

HALI ya “hewa” ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoani Arusha imechafuka  tena, baada ya Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Prosper Msoffe,  kupitia chama hicho  kuingia matatani akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kuingilia utendaji wa Halmashauri ya Jiji.

Tayari chama hicho ngazi ya Wilaya ya Arusha Mjini kimemwandikia barua Msoffe   ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Daraja Mbili  kikimtaka ajieleze  ndani ya siku saba kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya CHADEMA barua hiyo pia amenakiliwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk.Wilbroad  Slaa na wa Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa pamoja na Msoffe, madiwani wengne wanne pia wameandikiwa barua za kujieleza na kujibu tuhuma za kushirikiana na Naibu Meya huyo kukihujumu chama hicho.

Madiwani wanaotajwa kuandikiwa barua ya kujieleza na Kata zao kwenye mabano ni pamoja na Crispin Tarimo (Sekei), Reyson Ngowi (Kimandolu), Emmanuel Kessy (Kaloleni) na Malance  Kinabo  “Kaburu” (Themi).

Madiwani hao wanatuhumiwa kuunda “genge”  na  kumwunga mkono Naibu Meya ambaye anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kwa kufanya biashara  na Halmashauri ya Jiji la Arusha kinyume cha kanuni za viongozi wa umma.

Katika barua ya kumtaka Msoffe ajieleze  ambayo Raia Mwema imeona nakala  yake, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Arusha Mjini Martin Sarungi,  amemwagiza Naibu Meya huyo kujieleza ndani ya siku saba.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu  namba CDM/MD/06/FEB/2014 ya Februari 26, Msoffe anatuhumiwa  kuwa kwa nyakati tofauti ameingilia utendaji wa shughuli za Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa maslahi binafsi kinyume cha utaratibu.

Inasema barua hiyo: “Kwa nyakati tofauti umeingilia utendaji wa idara za Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa maslahi binafsi, kwa mfano, ununuzi wa mabegi na vitabu vya kumbukumbu (diary) ikiwa ni kinyume cha utaratibu”.

Tuhuma nyingine dhidi ya Naibu Meya huyo ni kutoa matamshi ya kukashifu, na kutoa lugha ya matusi na mwenendo wa kutia shaka kama Naibu Meya wa Jiji la Arusha kupitia chama cha CHADEMA.

Inaendelea barua hiyo: “Kwa nyakati tofauti umemkashifu na kumtukana Mwenyekiti wa Madiwani wa CHADEMA, Diwani wa Kata ya Ngarenaro, ndugu Isaya Doita”.

Aidha katika barua yake Sarungi anamalizia:”Barua  yako ya kujieleza itakuwa utetezi wako kwenye  Kamati tendaji ya Wilaya, Baraza la Mkoa, Baraza la Kanda ya Kaskazini na inatakiwa kufika ofisi ya Wilaya ndani ya siku saba”.

Kwa mujibu kwa kalenda siku saba  alizopewa Naibu Meya huyo ziliisha Machi 5 mwaka huu.

Taarifa zaidi kutoka ndani ya chama hicho cha upinzani zinadai kuwa Msoffe anakabiliwa na tuhuma za muda mrefu kuhusu kujihusisha na biashara na Halmashauri ya Jiji kinyume cha sheria na kanuni za uongozi wa umma.

Inadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti Naibu Meya huyo alipewa zabuni ndogo ya kununua mabegi  maalumu ya madiwani na mwanzoni mwa mwaka huu alipewa zabuni ya kuagiza vitabu vya kumbukumbu (diary) na idara ya manunuzi.

Kanuni zinakataza Madiwani kufanya biashara na Halmashauri wanazosimamia kwa lengo la kuepuka mgongano wa kimaslahi na CHADEMA  kinafahamika kwa misimamo ya kupiga vita ufisadi.

“Msoffe akitumia ushawishi na nafasi yake kama Naibu Meya, alipewa kibali cha kufanya manunuzi ya mabegi na vitabu vya kumbukumbu na maafisa wa idara ya manunuzi na ugavi kwa nyakati tofauti  mwaka 2013,”  kilieleza chanzo chetu.

Taarifa zinadai kuwa manunuzi hayo yalifanyika kupitia maduka mawili ya vifaa vya shule (stationary) yanayomilikiwa na Naibu Meya huyo ambayo yapo mjini Arusha.

Aidha, uamuzi wa kumwandikia barua ya kujieleza Naibu Meya huyo ulifikiwa baada ya kutokea mzozo katika kikao cha ndani ya chama mwishoni mwa mwezi Februari.

Katika kikao hicho inadaiwa  baadhi ya madiwani  waliibua tuhuma za ufisadi wa Msoffe ambaye anadaiwa kuwa mtu wa karibu na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.

Miongoni mwa tuhuma zilizoibuliwa  ni pamoja  kushiriki manunuzi ya vifaa vya Halmashauri  pamoja na kushirikiana na Meya Lyimo kufanya maamuzi   mbalimbali ya Halmashauri kwa maslahi yao ya kisiasa.

Aidha, kwa muda mrefu Naibu Meya huyo anatuhumiwa “kuunda ushirikiano haramu” na Meya wa Jiji la Arusha Gaudance Lyimo ambaye bado CHADEMA  kama chama  kinadai  hakimtambui.

Katika tuhuma zinazoelekezwa kwa Msoffe zipo zinazohusiana na mgogoro wa kampuni  ya Skytel iliyokuwa ikiendesha  mradi wa taa za barabarani ambapo pamoja na kampuni hiyo kukiuka mkataba Msoffe alijitokeza hadharani kuitetea.

Naibu  Meya huyo pia anatuhumiwa kuungana na baadhi ya viongozi wa CCM kumpiga vita aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji Zipora Liana ambaye baadaye alihamishiwa makao makuu ya Tamisemi  kwa maslahi yao ya kisiasa.

Inadaiwa kuwa baada ya kuibuliwa kwa tuhuma dhidi yake katika kikao kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri Msoffe alimshambulia kwa lugha ya matusi Mwenyekiti wa Madiwani wa CHADEMA Isaya Doita akimshinikiza aachie nafasi hiyo.

Akizungumzia  tuhuma zinazoelekezwa kwake Msoffe aliimbia Raia Mwema kuwa hajapokea barua yoyote kutoka kwa uongozi wa CHADEMA Wilaya ya Arusha.

“Kwanza sikuwepo Arusha kwa wiki mbili, nilikuwa kijijini kwangu  (Wilaya ya Mwanga) lakini sijaona barua yoyote inayonitaka kujieleza kutoka chama changu nipe muda wa saa moja nipitie ofisini kwangu nitakujulisha,” alisema.

Baada ya saa moja Msoffe alipiga simu na kusisitiza kuwa hakuna barua yoyote inayomtaka ajieleze iliyopokewa ofisini kwake.

“Sijaona barua. Na kuhusu tuhuma zinazotolewa ni kwamba mimi ni Naibu Meya wa Jiji naelewa kanuni na taratibu zinanizuia kufanya biashara  na Halmashauri, kwa maana hiyo sijwahi kufanyabiashara yoyote na Halmashauri ya Jiji,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Manunuzi na Ugavi wa Jiji la Arusha, Musa Musa, alisema ni kweli walitoa zabuni ndogo ya manunuzi hayo kwa mfanyabiashara mmoja ambaye hakumbuki jina lake.

“Ni kweli tulinunua hivyo vifaa ila siwezi kukumbuka, jina la kampuni iliyotumika na jina la mfanyabiashara huyo,” alisema Musa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Ephata Nanyaro  hakuwa tayari kukanusha wala kukubali chama chake kuandika barua hiyo kwa maelezo kuwa bado ni mapema kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya habari.

“Siwezi kusema chochote kwa sasa kwa kuwa sipo Arusha, ila masuala kama hayo ni ya kawaida katika vyama kwa watu kutofautiana mawazo na hatuwezi kusema kuna mgogoro,”alisema.

Nanyaro aliongeza kuwa atakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo  wiki ijayo atakapokuwa amerudi mjini Arusha na kusisitiza kuwa CHADEMA hakiwezi kuyumbishwa na suala dogo kama hilo.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger