Home » » Askofu ataka Katiba ya Zanzibar irekebishwe

Askofu ataka Katiba ya Zanzibar irekebishwe

Written By JAK on Tuesday, April 15, 2014 | 7:39 AM


http://nm-aist.ac.tz/staff/staff%20pic/Joseph%20Bundala.jpg

ASKOFU wa Jimbo Teule la Dodoma la Kanisa la Methodist, Joseph Bundala amesema ili kudumisha Muungano ni vyema Katiba ya Zanzibar irekebishwe.

Alisema anaomba katiba hiyo irekebishwe ili iwepo katiba moja ya nchi moja, ambayo inadumisha Muungano. Alisema hayo kwenye ibada ya kumsimika kuwa askofu wa kanisa hilo katika Jimbo la Dodoma.

Alisema hayo mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika ibada hiyo, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

“Ninamshauri Rais Jakaya Kikwete kuvunja Bunge Maalumu la Katiba kutokana na Bunge hilo kukosa mwelekeo na adabu. Inaonekana kama vile wapo kwa ajili ya kutafuna fedha za wananchi,” alisema Askofu Bundala.

Bundala alisema hafurahishwi na hali ya fujo na kutokuelewana ndani ya Bunge Maalum la Katiba, na kwamba hali hiyo inatokana na kukosewa kwa muundo wa kuwapata wajumbe.

Alisema kitendo cha kuwapata wajumbe wengi, ambao ni wana siasa ni tatizo kubwa katika upatikanaji wa katiba mpya.

“Rais hakutakiwa kuwateua wanasiasa wengi na zaidi, walitakiwa kuchaguliwa na wananchi, kwani hao ndio wanaojua zaidi matatizo yao,” alisema.

Kwa upande wake, Lukuvi aliendelea kupinga muundo wa Serikali tatu zilizopendekezwa kwenye rasimu ya pili ya katiba, kwa maelezo kuwa zitaifanya nchi kuingia kwenye gharama kubwa.

Lukuvi alisema Serikali inaendelea kusisitiza kuwa iwapo wananchi watakubali kuwepo kwa serikali tatu, kama zilivyopendekezwa katika rasimu ya pili ya katiba ni wazi kuwa nchi itatawaliwa na jeshi na kusababisha kuwepo kwa machafuko nchini.

“Kuna uwezekano mkubwa wa nchi ikatawaliwa na jeshi, pale Serikali moja itakaposhindwa kulipa mishahara; ama itakapotokea msuguano kati ya nchi moja na nchi nyingine, jambo ambalo ni hatari kwa nchi ambayo inaonekana kuwa amani,” alisema.

Waziri Lukuvi aliwataka Watanzania kuipuuza rasimu ya pili, ambayo ilionesha wazi kuwa na malengo ya Muungano wa Serikali tatu. Alisisitiza kuwa kuwepo kwa Serikali tatu ni kutaka nchi kuingia kwenye gharama kubwa.

Aliwataka waumini hao, kuliombea Bunge ambalo liko katika hali mbaya, kwani kuna watu wachache ambao sasa wanataka madaraka kwa nguvu huku nia yao kubwa ikiwa ni kuvunja Muungano na kudai kuwepo kwa serikali tatu.

Pia Waziri Lukuvi alisema upande wa Zanzibar pamoja na kutaka kuwa na nchi yao, lakini hawawezi kujitegemea bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.

Zamu ya Ngwilizi, Wassira

Kamati mbili za Bunge Maalumu la Katiba leo zinahitimisha kwa kuwasilisha maoni yake, kabla ya mjadala wa bunge zima kufanyika kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba kuanza rasmi wiki hii.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita ya Bunge Maalum la Katiba, Stephen Wassira na Mwenyekiti wa Kamati Namba Saba, Hassan Ngwilizi ndiyo wanahitimisha uwasilishaji wa maoni, baada ya kamati 10 kukamilisha mchakato huo wiki iliyopita, kabla ya mjadala bungeni kuanza kesho.

Mwenyekiti wa Kamati namba Sita, Wassira anawasilisha maoni ya wengi, akiwa tayari ameshaweka wazi kwamba wajumbe wengi wa Kamati yake, wanapendekeza Serikali Mbili huku wakipendekeza kumalizwa haraka kwa kero zilizopo.

Alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Wassira alisema wajumbe wengi wamependekeza kero zilizopo, zimalizwe haraka. Miongoni mwake ni, madai ya Tanzania Bara kuvaa koti la Muungano.

Kamati Namba Saba inayoongozwa na Ngwilizi, kama ilivyojitokeza katika kamati nyingine zilizotangulia, mawazo ya walio wengi yanatarajiwa kuibuka na mapendekezo ya serikali mbili.

Lissu

Licha ya wenyeviti hao wa kamati mbili, kuhitimisha uwasilishaji maoni ya wengi na wachache, pia Mjumbe Tundu Lissu leo anakamilisha kiporo cha ufafanuzi wa maoni ya walio wachache, kuhusu mjadala wa Kamati Namba Nne.

Ufafanuzi wa Lissu ulilazimika kuahirishwa Jumamosi baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta kuahirisha kikao cha Bunge Maalumu, kutokana na kukatika kwa matangazo ya Televisheni ya Taifa (TBC 1).

Atapewa nafasi ya kwanza na Mwenyekiti Sitta kukamilisha ufafanuzi wa maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne.

Sitta alisema alifikia uamuzi huo, kuondoa hisia zinazoweza kujitokeza kwamba kulikuwa na hujuma katika kukatika huko kwa matangazo ya TBC 1, wakati Lissu akitoa ufafanuzi wa maoni ya wajumbe walio wachache.

Alisema Bunge Maalumu la Katiba, liliingia mkataba na TBC 1 ili kurusha matangazo ya mijadala kwa lengo la kuwashirikisha wananchi katika mijadala hiyo.

Source : Habari Leo, Oscar Mbuza na Sifa Lubasi, Dodoma.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger