Home » » Zitto- Muungano ni imani si idadi ya Serikali

Zitto- Muungano ni imani si idadi ya Serikali

Written By JAK on Thursday, April 17, 2014 | 10:07 PM

http://media.tumblr.com/tumblr_ln70du2Xy11qa2ett.jpg
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Kabwe Zitto

Source : Habari Leo,Ikunda Erick, Dodoma

MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Kabwe Zitto amesema muundo wowote wa serikali uwe serikali moja, mbili au tatu unaweza kuvunja Muungano ikiwa hakutakuwa na muafaka wa pande zote mbili za Muungano.

Zitto alisema hayo jana bungeni wakati akichangia hoja za Kamati za Bunge Maalumu namba moja hadi 12, juu ya Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba na kuwataka wajumbe wa Bunge hilo kujadili hoja badala ya kutoa lugha za matusi.

“Mchakato huu tuufanye kwa kujadiliana kwa hoja, tusitukanane, muundo wowote wa serikali unaweza kuvunja Muungano, kikubwa ni kuafikiana maridhiano kutoka pande zote mbili za Muungano”, alisema Zitto.

Zitto ambaye hakusema anaunga mkono muundo upi wa Serikali, alisema jambo la msingi linalopaswa kufanywa na wajumbe wa Bunge hilo ni kufikia maridhiano ya pande mbili na sio kuendeleza ubaguzi na chuki ambavyo vimeanza kutawala miongoni mwa michango ya wajumbe wa Bunge hilo.

Kuhusu muundo wa Serikali, Zitto alisema ni vyema wajumbe wafikirie zaidi na kujifunza kutoka kwa nchi kama vile Somali, ambayo ilikuwa na muundo wa serikali moja lakini kwa kutoelewana ilivunjika na sasa hali sio nzuri nchini humo.

Kadhalika alitoa mfano mwingine wa Malaysia na kusema kama wajumbe wanataka serikali ya shirikisho, nchi hiyo ilikuwa na muundo huo, lakini kwa kutoelewana kwao ilivunjika na hadi sasa hakuna tafiti zilizothibitisha ni muundo upi wa serikali unaweza kulinda serikali isivunjike.

Alifafanua kuwa kinachoweza kulinda serikali ni kuwa na maridhiano ya pande zinazohusika na kwamba kama suala ni gharama za kuendesha serikali, ikiwa serikali itakusanya kodi ipasavyo, nchi itaendeshwa vizuri.

“Tuna uwezo wa kuendesha serikali za idadi yoyote ile, kwa kukusanya kodi, hiyo hofu ya kuendesha serikali ya Muungano kwa kutokuwa na fedha ni jambo la ukweli, lakini tunaweza kuboresha hizo hoja, ndiyo maana tumekuja, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?” Alihoji Zitto.

Katika hatua nyingine Zitto alisema ikiwa itaundwa serikali isiyo na maridhiano ya pande zote mbili za Muungano, gharama ya kuulinda Muungano huo ni kubwa kuliko uwepo wa kuwa na serikali tatu.

“Lazima tuwe na Muungano unaoeleweka, tuepuke lugha za matusi, chuki, ubaguzi, tunaelewa historia ya nchi yetu tubakie na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Zitto.

Naye mjumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, Issa Gafu alisema baadhi ya wajumbe wanaotaka Muungano uvunjike ni wachache ambao walikana uhuru wao wa mwaka 1964 na kamwe hawawezi kukubali Muungano.

“Hivi kama wewe uliukana uhuru wako mwaka 1964, utawezaje kukubali Muungano? Zanzibar inasumbuliwa na masuala ya uchumi na sio idadi ngapi za serikali,” alisema Gafu.

Akisisitiza hoja hiyo Gafu alisema, kama Zanzibar watatumia fursa zilizopo vizuri kwenye muundo wa serikali mbili wataendelea, lakini kudai muundo wa serikali tatu sio kwa manufaa bali ni kutaka kuvunja Muungano.

Akichangia hoja hiyo, mjumbe mwingine kutoka Zanzibar, Waziri Rajab Salum alisema mfumo wa serikali mbili ndio wenye manufaa kwa pande zote mbili na kwamba mitafaruku iliyopo Zanzibar haijaanza leo, bali ni wapinzani wa Muungano wa mwaka 1964.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger