Source Habari Leo - By Mgaya Kingoba, Dodoma
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imekemea tabia ya viongozi wa wilaya na mikoa wanaokataa watendaji wanaopelekwa kufanya kazi katika maeneo yao.
Mwenyekiti wa Taifa wa Wazazi, Abdallah Bulembo, amesema tabia hiyo haikubaliki, na viongozi hao hawana mamlaka ya kufanya hivyo.
Bulembo aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kabla ya kumkaribisha Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mizengo Pinda kufungua semina elekezi ya watendaji na viongozi wa ngazi ya Taifa, mikoa na wilaya inayofanyika mjini hapa.
“Halafu kuna tabia imeibuka ya viongozi wa wilaya na mikoa kukataa watendaji mnaoletewa huko kwenu.
Hoja hii ya kukataa watendaji inatoka wapi? “Mmeipata wapi nguvu hiyo? Halafu unamkataaje mtu akiwa getini pale? Si usubiri ufanye naye kazi uone alivyo ndipo uanze kulalamika,” alisema Bulembo.
Alisema tabia hiyo haikubaliki na haitavumiliwa ndani ya jumuiya hiyo, na kuwataka viongozi hao kuwapokea na kushirikiana na watendaji wanaopelekwa katika maeneo yao ya kazi.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Wazazi amesema watendaji waliokaa katika kituo kimoja cha kazi kwa miaka 20, watahamishwa karibuni.
“Mkitoka hapa mtaondoka na barua zenu. Tunawajua, msifikiri tumesahau,” alisema Bulembo na kuacha vicheko kutoka kwa wajumbe wa semina hiyo.
Aidha, alisema kwa watumishi waliofikisha umri wa miaka 60, pia watapaswa kustaafu kama sheria za utumishi zinavyoelekeza, na hakuna haja ya kukimbilia Makao Makuu ya Jumuiya, Dar es Salaam.
“Kwa wale waliozidi umri wa miaka sitini, tunawapongeza kwa kutanguliwa kuzaliwa, lakini hakuna haja ya kukimbilia Dar es Salaam, kujaza fomu, taratibu ziko wazi,” alisema Bulembo.
Semina hiyo ya siku tatu inayomalizika leo, mbali ya kuwahusisha makatibu wa wilaya, mikoa na wenyeviti wa wilaya, pia inawajumuisha wakuu wa shule za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi.
Post a Comment