Home » » SANGITO SUMARI NA WENZAKE 216 WASHINDWA KESI KATIKA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA ARUSHA

SANGITO SUMARI NA WENZAKE 216 WASHINDWA KESI KATIKA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA ARUSHA

Written By JAK on Monday, February 24, 2014 | 11:07 PM

Source - Afisa Habari wa Jiji Nteghenjwa Hosseah

Na HATIMAYE Halmashauri ya Jiji la Arusha imevunja nyumba zake 338 baada ya kushinda
 kesi iliyofunguliwa na wapangaji Sangito Sumari na wenzake 216 katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha.

Oparesheni hiyo inayojulikana kama “Oparesheni Mongela” ilianza Saa 12 asubuhi juzi kwa kuvunja nyumba 56 eneo la Kilombero, nyumba 198 eneo la Kaloleni na nyumba 84 katika eneo la Themi.

Wengi walitegemea kuibuka vurugu wakati wa uvunjaji nyumba lakini hadi mchana hapakuwa na pingamizi kwa wapangaji badala yake wenyewe walihamisha vitu vyao mapema jana asubuhi kabla ya zoezi la kuvunja kuanza.

Hata hivyo kuvunjwa kwa nyumba hizo kumeleta neema kwa baadhi ya watu wakiwamo vijana wanaokusanya vyuma chakavu kuvamia maeneo hayo na kuokota kila aina ya chumba au kitu ambacho waliamini kinaweza kuuzwa na kuwapatia fedha.

Akiwa eneo la Kaloleni baada ya kukamiliza kuvunjwa nyumba za Kilombero, Mkuu wa wilaya ya Arusha Mongela alisema, ‘Oparesheni Mongela’ ilipata baraka zote za viongozi wa serikali wanasiasa wakiwamo madiwani wote Mbunge na Meya wa Jiji.

“Niwashukuru wananchi wa Jiji la Arusha kwa ushirikiano tofauti na tulivyotarajia. Wapangaji wenyewe wametusaidia sana, japo kuwa kuna uchungu wa kuhama eneo ambalo wamelizoea.

“Madiwani wa vyama vyote wametoa ushirikiano mkubwa katika hili tumekuwa pamoja, tumezungumza lugha moja na tumetembea pamoja. Mbunge tumezungumza naye akiwa Dodoma Bunge la Katiba akasema angependa kuwapo.

“Kwa niaba ya kiongozi mwenzangu kwasababu hayupo nisema kwamba nayeye ametoa ushikiano mkubwa kabisa wa kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa na tunakuwa na Jiji la Arusha lenye taswira ya Geneva ya Afrika,” alisema Dc Mongela. 

Alisema kuvunjwa kwa maeneo hayo kutarahisisha uwekezaji mkubwa zaidi ambao unatarajiwa kufanywa katika siku za hivi karibuni ambapo uwezo wa kiuchumi kwa Jiji la Arusha unatarajiwa kuongezeka ikiwani ni pamoja na kuweka madhari kuwa ya kisasa zaidi.

Baadhi ya wananchi kwa upande wao wakizungumzia kuvunjwa kwa nyumba hizo ambazo zimekuwa na mvutano wa miaka mingi tangu mwaka 2010 wapo waliopongeza huku wengine wakipinga zoezi hilo na kudai ni uonevu mkubwa umefanyika.

Mwananchi Zainab Jabir aliyekuwa mpangaji wa nyumba hizo za Manispaa eneo la Kaloleni alisema, lawama na laana zake anazipeleka kwa wanasiasa waliokuwa wakiwahamasisha wasihame kwenye nyumba hizo.

“Kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani wa Kata nne, tukiwa eneo la Ilboru Naibu Meya wa Jiji la Arusha alituhakikishia kwamba notisi zimesimamishwa hivyo wapangaji tusubirie mpaka tamko litakapotoka.

“Hatujakataa kuondoka ila tungepewa siku tatu tujiandae ona hapa vitu vimevunjika watoto hawajui watakula nini, wazee hawana mahali pa kupumzika. Na wanasiasa wamechangia sisi kuondoka bila utaratibu mbona marehemu Mzee Kileo (Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Arusha) alikuwa anatutetea?”Alihoji Zainab na kuendelea:

“Nilichojifunza ni kwamba hapa kuna uonevu mkubwa sitakaa nimpigie kura mwanasiasa yoyote chini ya jua,” alidai.

Naye muathrika mwingine Hassani Mbaga aliyekuwa akiishi eneo B Kaloleni alisema kwa upande wake alilidhika kuvunjwa kwa nyumba hizo kutokana na ukweli kwamba zilikuwa zimefika mwisho wa matumizi ya kibinadamu.

“Tumeridhika japo tulichelewa kutii agizo. Ukifuatulia kwa makini kiafya nyumba hizi hazikufaa kuishi binadamu zilifikia mwisho wa matumizi yake na hazikuwa na vyoo maji.

“Kwa upande mwingine mpaka kuchelewa kuondoka hapa wanasiasa wamechangia sana kutuotosha hasa wabunge na madiwani kwani walikuwa wakituambia tusiondoke, japokuwa sasa hasara imerudi kwa mtu mwananchi wa kawaida,” alisema Mbaga.

Akitoa ufafanuzi wa kisheria katika suala hilo Mwanasheria wa Jiji la Arusha Kiomoni Kibamba alisema uamuzi huo umekuja baada ya kuwapo kwa majibizano ya muda mrefu baina ya wapangaji wao 216 waliokuwa wakiongozwa na Sumari.

Alisema kwa miaka mingi Halmashauri hiyo ilipanga kuyaendeleza maeneo hayo kwa kuvunja nyumba za zamani na kukaribisha uwekezaji mkubwa lakini waliokuwa wapangaji wao waligoma na kukimbilia mahakamani.

Kiomoni alisema kabla ya kukimbilia mahakamani kufungua kesi waangaji wao waliweka masharti magumu matatu dhidi ya mwenyewe nyumba ambapo walitaka kupewa fidia ya kukaa kwenye nyumba hizi.

Alisema masharti mengine yalikuwa ni Halmashauri iwajibike kuwatafutia viwanja kwingine ili wakajenge na sharti la mwisho alilitaja kuwa waangaji hao walitaka kupangishwa kwenye uwekezaji utakaofanywa,” alisema Mwanasheria Kiomoni.

Alisema baada ya kushindwana ndipo wapangaji hao walipofungua kesi mahakamani, ambapo kesi hiyo iliendelea kusikilizwa hadi ilipotolewa uamuzi juzi.

“Tumewahi kuiomba Mahakama iwape notisi ya miezi 6 kuanzia Januari 11, Mwaka 2013 wakae bila malipo wakati wakitafuta nyumba kwingine. Juni 10, Mwaka 2013 ilikuwa ukomo wa notisi iliyotolewa hivyo Jiji lilitaka kuvunja nyumba zake.

“Wapangaji walikwenda Mahakama Kuu wakafungua kesi namba 23 ya 2013 hivyo ilitolewa amri ya zuio la muda hadi hapo madai yao yatakaposikilizwa. Lakini na sisi tuliweka pingamizi kwamba hapakuwa na mgogoro kati yetu na wapangaji.

“Baada ya kusikilizwa kwa mashaurio hayo Februari 21, Mwaka huu Jaji Moshi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha alitoa uamuzi kuwa mapingamizi yangu niliyoweka yalikuwa na msingi hivyo alitupilia mbali madai ya wapangaji,” alisema Kiomoni.








KILA KITU KILIKUWA NA KAZI KAMA INAVYONEKANA HAPO KWENYE PICHA
VIJANA WANAONUNUA BIDHAA ZA CHUMA CHAKAVU WAKIWA KIBIASHARA ZAIDI
KUFA KUFAANA , KIJANA ALIYESHIKILIWA AMWENYE SHATI JEUSI AKIWA AMEBAMBWA ANAIBA MALI ZA WAPANGAJI WALIOKUWA KATIKA ZOEZI LA KUHAMISHA MALI ZAO
MAFUNDI WA TANESCO NAO WALIKUWEPO KUHAKIKISHA HAPATOKEI HITILAFU YEYOTE KATIKA ZOEZI HILO KATIKA KATA YA KALOLENI
WENGI WA WAPANGAJI WALIAMUA KUNGOA MADIRISHA NA MILANGO NA HATA VIGAE NA KUZIACHA KAMA ZINAVYONEKANA
MAGARI AINA YA FUSO NA AINA YA PICK UP NAZO ILIKUWA NI SIKU NZURI KWA BIASHARA KWAO

Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger