Mwenyekiti ataka Wajumbe kuvumiliana Na Mwandishi Wetu, Dodoma MWENYEKITI wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho amewataka wajumbe wa Bunge hilo kuvumiliana na kuwa wastaarabu wakati wa mijadala mbalimbali. Akiahirisha kikao cha kazi
MWENYEKITI wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho amewataka wajumbe wa Bunge hilo kuvumiliana na kuwa wastaarabu wakati wa mijadala mbalimbali.
Akiahirisha kikao cha kazi jana mjini hapa hadi Jumatatu asubuhi, Kificho ambaye ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, alisema wajumbe hao hawana budi kuvumiliana kwa nia ya kuwa na mijadala mizuri yenye nia ya kujenga na kuwa na Katiba nzuri kwa maslahi ya Watanzania.
“Nawaombeni sana, tuwe wavumilivu na wastaarabu. Sote humu ni watu wazima, watu makini, ni vyema kuwa na tabia ya kuvumiliana. Si vizuri hata kidogo, mwenzako anapozungumza kumzomea au kufanya vurugu zozote,” alisema Kificho.
Alisema ni vyema wajumbe wakajitahidi kuifanya kazi iliyowapeleka kwa weledi na kuacha mambo ambayo yatawakwaza, yakiwamo ya kutozungumza bila utaratibu ndani ya Ukumbi wa Mikutano.
Kauli ya Mwenyekiti huyo wa Muda imekuja baada ya jana kuwapo na sintofahamu na kauli zenye kuashiria majibizano baina ya wajumbe wakati wa kuchangia maoni kutokana na maelezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Frederick Werema.
Werema alikuwa akiwapitisha wajumbe katika baadhi ya mambo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Toleo la Mwaka 2014 kwa nia ya kuwapa ufahamu zaidi wajumbe hao.
Lakini wakati wakitoa maoni yao au kumwuliza maswali Mwanasheria Mkuu huyo, baadhi ya wajumbe walionekana kujibu wenzao au kutoa lugha za kuudhi au za kuhusisha vyama vyao.
Mjumbe Christopher Ole Sendeka ambaye ni Mbunge wa Simanjiro katika mchango wake alimtaja waziwazi Mjumbe Tundu Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, kuwa alikuwa anataka kupotosha kuhusu sheria hiyo kwani alishiriki katika vikao vya Bunge na vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala.
Katika maoni yake, pamoja na mambo mengine, Lissu ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, alisema Sheria hiyo imeruhusu Bunge Maalumu la Katiba kuifuta Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, suala ambalo lilizua miguno na kumfanya Sendeka alipopewa fursa ‘kumsuta’ mjumbe mwenzake.
Aidha, Mjumbe Ismail Aden Rage ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini lakini alijitambulisha kama Rais wa Klabu ya Simba, alimvaa Mjumbe Profesa Haruna Lipumba, akikosoa nukuu aliyodai ni ya hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, akisema hakuitoa Warioba, bali Mwenyekiti huyo wa Chama cha Wananchi (CUF), ameinukuu kutoka gazeti la Mawio.
Aidha, Mjumbe Mussa Haji Kombo (CUF), ambaye ni Mbunge wa Chakechake, alipopewa nafasi ya kuzungumza, akaitumia kumshambulia Rage akisema Mwenyekiti wake, bila kumtaja jina Profesa Lipumba, alikuwa sahihi na kwamba kwa kauli ya Rage, ndio maana inaonekana klabu za michezo haziendelei.
Hakufafanua lakini alimlenga Rage kwa nafasi yake ya uenyekiti wa Simba. Lakini wakati mbunge huyo wa CUF akizungumza huku kila mara akitaja neno ‘Mwenyekiti wangu,’ Mjumbe Sadifa Juma Khamis, ambaye ni Mbunge wa Donge, alikuwa akiwasha kipaza sauti chake na kuomba mwongozo kuhusu utaratibu kwa Mwenyekiti wa Muda, Kificho.
Hata hivyo, zaidi ya mara tatu Kificho alimkatiza na kusema mwongozo huo kuhusu utaratibu angepatiwa nafasi baadaye, jambo ambalo halikutokea.
Kwa hali ya kawaida, ilitarajiwa kuwa Sadifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), angesema kwa mujibu wa Bunge hilo, hakuna Mwenyekiti wa chama, bali Mjumbe, hivyo Profesa Lipumba alipaswa kurejewa kama Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Aidha, bado kulikuwa na mzozo wa nani azungumze, kwani baadhi ya wajumbe walikuwa wakiwasha vipaza sauti vyao na kuzungumza kabla ya kupewa ruhusa na Mwenyekiti, hivyo kusababisha zogo.
Lakini inatarajiwa kuwa baada ya kupitishwa kwa Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, angalau kutakuwa na ustaarabu hasa ikizingatiwa kuwa Kanuni hizo zimeweka adhabu kwa wanaokwenda kinyume.
Post a Comment