Home » » Vimini, vitopu marufuku Uganda

Vimini, vitopu marufuku Uganda

Written By JAK on Thursday, February 20, 2014 | 9:02 PM

 http://www.habarileo.co.tz/images/RaisMuseveni.jpg

RAIS Yoweri Museveni amesaini sheria ambayo inaharamisha mavazi yasiyo ya heshima na picha za utupu. 

Pia, wanawake wamepigwa marufuku kuvaa nguo fupi - vimini na blauzi fupi – vitopu, ambavyo vinashawishi hisia za ngono, isipokuwa kama vivazi hivyo vitatumika kwa madhumuni ya kutoa elimu au matibabu au kutumika kwenye michezo na utamaduni.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Habari jijini hapa juzi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maadili, Mchungaji Simon Lokodo, alisema Rais alisaini Muswada huo kuwa sheria Februari 6, miezi miwili baada ya kupitishwa na Bunge Desemba mwaka jana.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, sasa itaundwa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Ukiukwaji wa Maadili ya Nchi, ambayo itakuwa na wajibu wa kubaini, kukusanya na kuharibu vitu vyote vinavyohusiana na ponografia (picha au maandishi yenye kutia ashiki).

Kamati hiyo, ambayo wajumbe wake watatoka sekta mbalimbali zikiwamo tasnia za habari na burudani, pia itatoa huduma za kurekebisha tabia kwa waathirika wa ponografia.

Sheria hiyo dhidi ya ponografia, inatengua na kuchukua nafasi ya Kifungu cha 166 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na kupanua wigo wa tafsiri ya sheria ya ponografia na kuiharamisha.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ponografia inamaanisha “chochote kitakachotolewa kupitia chapisho, maonesho, filamu, teknolojia ya mawasiliano au kwa njia nyingine yoyote, kinachoonesha mtu akiwa katika tendo halisia au maigizo ya ngono au kuonesha sehemu za siri za mtu kwa ajili ya kusababisha ashiki.”

Waziri Lokodo pia alitaja matangazo mafupi ya ngono maarufu kama bimansulo, video au picha za ngono kwa watoto, na wanamuziki, hususan wasanii wa kike, ambao hucheza wakiwa wamevalia nguo fupi, kwamba navyo vimepigwa marufuku.

“Hatupendi mwonekane katika hali ambayo inavuta hisia za watu wengine. Kuweni na staha na nguo zenu zikuonesheni kuwa watu wenye staha,” alisema Lokodo.

Alipotakiwa kufafanua kuhusu uvaaji usio na staha, Waziri alisema: “Kama utavaa vazi ambalo linatatiza fikra na kushitua watu wengine hususan wa jinsia tofauti, umevaa vibaya na tafadhali harakisha kubadilisha vazi lako.”

Vituo vya habari navyo vimepigwa marufuku, kuchapisha picha za watu wawili wakibusiana au wanawake waliovaa vibaya kama wanaoonekana katika klabu za usiku, kwa mujibu wa Patricia Achan-Okiria, Ofisa Mkuu wa Sheria katika Wizara ya Maadili.

Waziri huyo alielezea wasiwasi unaooneshwa na wabia wa maendeleo juu ya muswada wa kupinga ponografia, kama jambo ambalo halitaweza kuiondoa ofisi yake kwenye mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger