Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) atafanya ziara ya kikazi ya siku tano katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari, 2014. Ziara ya Mhe. Membe inakuja kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi.
Mhe. Membe anafanya ziara hiyo nchini China kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na China. Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Membe atafuatana na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Ziara hii pia ni muendelezo wa maeneo ya utekelezaji baada ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping aliyoifanya hapa nchini tarehe 24 na 25 Machi, 2013 na baadaye ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda nchini China mwezi Oktoba, 2013.
Akiwa nchini China, Mhe. Membe atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China tarehe 25 Februari 2014. Siku hiyo hiyo Mhe. Membe atamtembelea Makamu wa Rais wa China, Mhe. Li Yuanchao kwa lengo la kumsalimia na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Biashara wa China, Mhe. Gao Hucheng.
Aidha, tarehe 26 Februari, 2014 Mhe. Membe atatembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Poly Technologies yaliyopo katika mji wa Shenzhen na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kampuni hiyo kabla ya kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchant Holdings International ambako atapokea taarifa ya maandalizi ya kuanza kwa mradi wa Ujenzi wa Bandari katika eneo la Mbegani huko Bagamoyo.
Mhe. Membe pia atapata fursa ya kutembelea Kampuni ya HUAWEI ili kujionea shughuli mbalimbali. Kampuni ya HUAWEI ina Mkataba na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya hapa nchini kuhusu Elimu kwa Njia ya Mtandao (e-Education) kwa Shule za Sekondari.
Vile vile tarehe 27 Februari, 2014, Mhe. Membe atautembelea Mji maarufu wa biashara wa Guangzhou na kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi mjini hapo. Mhe. Membe atatoa taarifa kuhusu hali ya uchumi, siasa na masuala ya jamii yalivyo hapa nchini kwa sasa pamoja na kutoa taarifa ya maendeleo ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Waziri Membe pia atatembelea Eneo la Viwanda la Huadu tarehe 28 Februari, 2014 kabla ya kurejea nchini tarehe 1 Machi, 2014.
IMETOLEWA NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
24 FEBRUARI, 2014
Post a Comment