Home » » NHIF yapongezwa kwa huduma za upimaji Afya bure

NHIF yapongezwa kwa huduma za upimaji Afya bure

Written By JAK on Saturday, February 1, 2014 | 5:42 AM



Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia kipeperushi cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kinachoelezea fao la wastaafu wakati alipotembelea banda la Mfuko huo katika maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo Tengeru.
 Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nyerembe Munasa Sabi akiteta jambo na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Kagenzi Trasias baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa Maofisa wa NHIF kuhusiana na namna ya kujiunga na Mfuko huo kwa wanafunzi wa Vyuo vikuu.
 Ofisa wa NHIF, Paul Minzi akiendelea na zoezi la kupima uzito na urefu kwa wananchi waliojitokeza kupima katika banda la Mfuko huo.
 Upimaji wa afya za wananchi sambamba na ushauri wa namna ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza ukiendelea.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Anna Maembe akiteta jambo na Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma wa NHIF kuhusiana na ushiriki wa Mfuko huo kwenye maadhimisho hayo.
 Wananchi wakiendelea na kujua hali ya afya zao.
 Wananchi mbalimbali wakisubiri kupata huduma ya kupima afya zao kwenye banda la NHIF ambalo lilitoa huduma za upimaji bure.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

MAKAMU wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa juhudi zake za kutoa huduma ya upimaji wa afya za wananchi katika maeneo mbalimbali hatua inayowasaidia wananchi kutambua hali ya afya zao.

Pongezi hizo amezitoa baada ya kupata maelezo kutoka kwa Meneja wa NHIF, Arusha, Anicia Ng’weshemi ya namna Mfuko huo ulivyoa huduma za upimaji wa afya bure katika maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo Tengeru.

“Kazi mnayoifanya ni nzuri kwani matatizo kama sukari, shinikizo la damu na uzito uliozidi yanazidi kuwa tishio hivyo mmefanya kazi nzuri,” alisema.

Katika maonesho hayo, zaidi ya watu 600 wamenufaika na huduma hizo ambazo zilikwenda sambamba na elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa.

NHIF imekuwa ikiendesha upimaji katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kuwasaidia wananchi kufahamu afya zao lakini pia kuwapa ushauri wa namna ya kujikinga na maradhi yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanaongezeka kila kukicha.

Kundi kubwa lililopatiwa huduma katika maadhimisho haya ni Maofisa Maendeleo ya Jamii wa nzima ambao walikuwa na Mkutano Mkuu chuoni hapo, wanachuo pamoja na baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na chuo, maadhimisho yaliyofungwa na Makamu wa Pili wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Mbali na huduma za upimaji, NHIF pia ilikuwa na dawati la elimu kwa umma ambalo kazi yake kubwa ilikuwa ni kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa kujiunga na NHIF, Mfuko wa Afya ya Jamii na Tiba kwa Kadi, kutoa ufafanunuzi wa masuala mbalimbali kwa wanachama, haki na wajibu kwa mwanachama wa NHIF wakati wa kupata huduma.

Wakizungumza katika banda la Mfuko huo wanachama na wananchi wengine waliofika kwa lengo la kupata huduma walisema huduma zinazotolewa na Mfuko ni nzuri kwa kuwa zimelenga kumkomboa mwananchi wa kawaida hasa katika kipindi hiki ambacho gharama za matibabu zimekuwa ni kubwa.

“Hiki kitendo mnachofanya cha kuja kutupima afya zetu na kutupatia ushauri wa namna ya kuepukana na magonjwa haya ni kitendo cha kupigiwa mfano…mmeona umuhimu wa kutusaidia wananchi kujikinga badala ya kusubiri tuumwe hivyo ni vyema huduma hizi mkazipeleka katika maeneo mengi ili kuwasaidia wengi zaidi,” alisema Joseph Athanas mkazi wa Tengeru.

Hata hivyo kwa upande wa wanachama ambao wananufaika na huduma za NHIF walisema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto za hapa na pale zinazoukabili Mfuko lakini hawakusita kupongeza maboresho mbalimbali ya huduma yanayofanywa na Mfuko hususan fao la wastaafu ambalo limelenga kuwaenzi na kuwasaidia katika maisha yao yote.

Akitoa ushauri wa jumla kwa wananchi, Ofisa Udhibiti Ubora wa NHIF, Dk. Peter Nyakubega, alisema kuwa ni vyema wananchi wakawa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara hali itakayowasaidia kujitambua kutokana na ukweli kwamba magonjwa haya kwa sasa yanaongezeka na matibabu yake ni ya ghari.

Alisema kuwa magonjwa haya yanasababisha na hali halisi ya maisha yaliyopo sasa hivyo ni vyema mkakati wa kufuatilia afya ukawa kwa kila mwananchi kwa kuwa bila kuwa na afya njema hata maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla yatayumba.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger