Home » » SERIKALI INA NIA NA BWAWA LA KIDUNDA - NAIBU WAZIRI WA MAJI

SERIKALI INA NIA NA BWAWA LA KIDUNDA - NAIBU WAZIRI WA MAJI

Written By JAK on Tuesday, February 11, 2014 | 8:23 PM

Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, amesema Serikali ina nia na bwawa la Kidunda na watahakikisha wanautekeleza mradi huo kama ilivyopanga.

Mhe. Makalla amezungumza hayo jana wakati alipotembelea kijiji cha Bwira Chini ambacho pamoja na Bwira Juu ni moja ya vijiji vitakavyopisha ujenzi wa bwawa hilo kubwa, kuongea na wananchi ambao wamekua katika hali ya sintofahamu kuhusu utaratibu wa kuhama katika makazi yao kwa ajili ya kupisha ujenzi huo.

“Serikali ina nia na bwawa la Kidunda, ila yapo mapungufu katika kutekeleza mradi huu na kama Serikali tunazipokea changamoto hizi na tutazifanyia kazi. Nitahakikisha hatua sahihi zinachukuliwa ili utekelezaji wa kazi hii uanze”, alisema Naibu Waziri.

“Naagiza DAWASA na Halmashauri ya Wilaya walitafutie ufumbuzi suala hili na watoe tamko baada ya siku kumi na nne na ninaomba wananchi waelewe Wizara ya Maji ina taasisi kama DAWASA inazozielekeza kufanya kazi kwa niaba yake, hivyo naomba msivilaumu wala kutokubaliana na maamuzi yake, bali mviheshimu na kuvipa ushirikaiano wa kutosha ili vitekeleze majukumu yake vyema”, aliongeza Mhe. Makalla.

Pia, Naibu Waziri alisema atazungumza na Rais, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili Serikali itafute fedha za dharura ili kufanikisha mradi huo kama moja ya kutimiza sera na mipango yake iliyojiwekea.

Aidha, Mbunge wa Morogoro Kusini na Bwira Chini ikiwa ni moja ya kijiji kilichopo katika jimbo hilo, Innocent Kalogeris, aliyeambatana na Mhe. Makalla katika ziara hiyo alimshukuru Naibu Waziri wa Maji kufika na kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu.

“Nashukuru Mhe. Makalla kwa kufika na kuzungumza na wananchi wa Bwira Chini ili kupata suluhisho la ujenzi wa mradi huu wa Bwawa la Kidunda. Maombi yangu ni kuomba tathmini ya fidia kwa wananchi ifanyike kama ulivyoagaiza, ili wananchi wajue stahiki zao sahihi ili waweze kwenda kwenye maeneo mengine waliyopangiwa na kupisha mradi huu mkubwa na wenye manufaa mengi kwa nchi yetu kuanza”, alisema Mhe. Kalogeris.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Maji, pia alifuatana na Mbunge wa Morogoro Kusini-Mashariki, Lucy Nkya, ambaye alikuwa akiwawakilisha wananchi wa Bwira Juu ambao nao pia wanatarajiwa kuhama kupisha ujenzi huo. Ujenzi wa Bwawa la Kidunda ni mradi mkubwa uliopangwa kujengwa mkoani Morogoro ili kuweza kutoa maji ya kutosha kuhudumia mkoa wa Dar es Salaam na kumaliza changamoto za maji zinazikumba jiji hilo.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akisikiliza ripoti ya maji ya Wilaya ya Morogoro katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, kushoto ni Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris.
Mbunge wa Morogoro Kusini-Mashariki, Lucy Nkya akizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla wilayani Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi akizungumza katika mkutano wa Naibu Waziri wa Maji katika ziara yake wilayani hapo.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akizungumza na wananchi wa Bwira Chini katika ziara yake kijijini hapo, kushoto ni Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi.
Wakazi wa kijiji cha Bwira Chini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla (hayupo pichani), wakati wa alipotembelea kijiji hicho katika ziara yake wilayani hapo.
Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bwira Chini katika ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla katika jimbo lake, wilayani Morogoro.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger