Home » » Wasomi washikilia Serikali moja

Wasomi washikilia Serikali moja

Written By JAK on Wednesday, February 19, 2014 | 8:09 PM

 http://habarileo.co.tz/images/BungeKatiba.jpg
 (Source - Habari Leo by     Halima Mlacha) WASOMI wa Taasisi ya Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP) , wametoa msimamo wao na kutaka mfumo wa Serikali moja, huku wakipinga wa Serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Marekebisho ya Katiba.

Pia wasomi kutoka Kenya na Afrika Kusini, wameshauri Watanzania kuachana na mjadala wa mfumo wa idadi ya serikali na badala yake, watengeneze Katiba itakayojali maslahi ya wananchi, kujenga umoja na kutatua matatizo yao ya muda mrefu.

Akizungumza kwa niaba ya wasomi hao waliohudhuria mjadala wa siku mbili wa upatikanaji wa Katiba Bora Tanzania ulioandaliwa na ESAURP, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Ted Malyamkono, alisema katika nchi inayoendelea kama Tanzania, kamwe haiwezi kuendelea ikiwa na mfumo wa Serikali tatu au nne.

“Sisi wasomi msimamo wetu na mapendekezo yetu katika Katiba hii ni Serikali moja, Serikali hii ndiyo itakayojenga umoja wa Watanzania na kuwatatulia matatizo yao ya muda mrefu, nchi kama Tanzania kamwe haiwezi kuendelea kwa mfumo wa Serikali tatu au nne,” alisema Malyamkono.

Alisema kwa sasa mfumo wa Serikali mbili unaotekelezwa kupitia Katiba ya mwaka 1977 una walakini, ambapo nao una ubaguzi kwa kuwa upande wa Zanzibar umeonekana kunufaika zaidi na Muungano kuliko Bara.

“Tanzania Bara wanatumia fedha nyingi kujijenga na faida tunatumia wote na Wazanzibari wakati Bara hawanufaiki na chochote kutoka Zanzibar, hii ni kero kubwa kwetu, lazima Katiba iangalie mambo kama haya ambayo utatuzi ni Serikali moja tu,” alisisitiza.

Profesa Bonaventure Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na kuunga mkono msimamo wa mfumo wa Serikali moja, pia alisisitiza kuwa hoja ya kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba ilianzishwa na wasomi tangu miaka 20 iliyopita na si wanasiasa kama inavyodhaniwa.

Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine, Dk Charles Kitima, alisema msomi yeyote duniani akiulizwa achague aina ya serikali kwa ajili ya nchi yake, lazima achague mfumo wa Serikali moja kwa kuwa ni kiungo cha umoja, amani na utulivu kwa nchi yoyote.

Alisema Tanzania ni vema ikajikita katika mfumo wa Serikali moja kwa kuwa ndiyo matakwa ya waasisi wa nchi hii; Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

“Waasisi hawa matakwa yao yalikuwa ni kuwa na Serikali moja itakayounganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja, walianza na Serikali ikiwa ni utaratibu wa kujiandaa tu na lengo liwe hapo baadaye nchi hizo kuwa kitu kimoja, sisi leo kweli ni haki kuja na mfumo wetu?” Alihoji.

Awali akiwasilisha mada kuhusu uzoefu wa Kenya katika mchakato wa kuanzisha Katiba mpya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sera Afrika iliyoko Nairobi, Kenya, Profesa Peter Kagwanja, alisema Tanzania ina uwezo wa kutengeneza Katiba bora yenye maslahi ya wananchi wake, iwapo matakwa ya wananchi yatazingatiwa hasa matatizo yao.

“Sisi mchakato wetu ulichukua muda mrefu tangu mwaka 1988 na Katiba ikapatikana mwaka 2010, lengo lilikuwa si kuwa na Katiba mpya ili kujiendeleza kiuchumi, lengo lilikuwa ni kuwa na Katiba mpya ili kukabiliana na matatizo ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa, Tanzania inaweza kuwa na Katiba itakayoangalia matatizo yao,” alisisitiza.

Derrick Marco wa Taasisi ya Demokrasia Afrika (IDA) kutoka Afrika Kusini, akizungumzia uzoefu wa Afrika Kusini katika mchakato wa Katiba mpya, alisema si lazima Watanzania kujikita katika eneo la idadi ya mfumo wa Serikali na kwamba jambo la msingi ni kuwa na Katiba itakayojali maslahi ya wananchi na itakayodumu kwa muda mrefu.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger