Home » » Stephen Wasira asababisha kicheko kwa waombolezaji katika maziko ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa

Stephen Wasira asababisha kicheko kwa waombolezaji katika maziko ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa

Written By JAK on Monday, March 31, 2014 | 6:02 PM


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira alisababisha kicheko kwa waombolezaji katika maziko ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa baada ya kulalamikia masharti yanayoambatana na safari ya kwenda peponi.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Mara katika Ibada ya Maziko iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Tuppa, Kilosa mjini, Morogoro, Wasira alisema watu wote waliohudhuria hapo wanataka kwenda peponi lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari hiyo.

“Baba Askofu Mkude (Telesphor), ukiuliza nani anataka kwenda peponi, wote hapa watanyoosha mikono, lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari ya kwenda huko. Kila mtu anaona ugumu wa hayo masharti ukiwemo wewe Baba Askofu,” alisema Wasira huku umati uliokuwepo ukiangua vicheko.

Alisema kifo hakizoeleki wala hakizuiliki na kwamba hakuna anayeweza kuchakachua siri ya Mungu kuhusu uhai wa maisha ya wanadamu. Wasira pia alitumia fursa hiyo kuwaombea wafiwa wapate faraja katika kipindi hicho kigumu.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana jioni akizungumza na waombolezaji wakati wa ibada hiyo, alisema amemfahamu Tuppa tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya kwa mara ya kwanza.

“Tuppa alikuwa mtumishi Serikalini kwa muda wa miaka 42 na katika muda wote huo, miaka 21 ya utumishi wake alikuwa akihudumia wananchi kama Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Alikuwa mtu mwema, aliyejali watu na wala hakuwa na tamaa za hovyo hovyo,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza.

“Kumpoteza mume na baba ni mtihani mkubwa lakini mkimtumaini Mwenyezi Mungu mtafaulu,” alisema Waziri Mkuu na kuwasihi mjane wa marehemu Tuppa pamoja na watoto wasisononeke wanapopatwa na jambo na wasisite kumuona Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yeye binafsi au Rais Jakaya Kikwete, kwa msaada zaidi.

Awali, katika Ibada ya Misa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude aliwataka watu waliohudhuria maziko hayo kufanya toba kama njia ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.

“Ninawaomba kila mmoja mahali hapa afanye toba, awe mkweli, asifanye uchakachuaji... kila mtu kwa imani yake aache mabaya na atende mema kama ndugu yetu John Tuppa ambaye alijitoa na kufanya zaidi kwa ajili ya wengine.

“Je, mnawaongozaje watu katika ofisi zenu katika ngazi mbalimbali, iwe ni wizarani, mkoani, wilayani hadi kwa mtendaji wa kijiji? Je, unawafanyaje watu katika biashara unayofanya? Je, unawadhalilisha kwa kuwauzia vitu vibovu? Je, unawauzia dawa za kulevya?” alihoji Askofu Mkude.

Aliwataka watu kila mmoja kwa imani yake kuendelea kuombea mchakato wa Katiba ipatikane Katiba bora zaidi. “Tuna wajibu kama wacha Mungu tuwaombee wajumbe wa Bunge Maalumu ili kazi ile ifanyike sawa na mapenzi ya Mungu. Tusipowaombea watafanya vitu vya ajabu,” alisisitiza.

Maziko hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, baadhi ya mawaziri, wabunge wa Mara na Morogoro, wakuu wa mikoa mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.

Tuppa alizaliwa Januari mosi, 1950.

Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011.

Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu watano

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh2HEeLe-_Wu5Ui2Q20J6j4FmVSIq6jAkgHDBRKAmxKBsUa_sNzHFXA2Rl6kyEDu8qZdYGF8uPEBdAiXm8MzRd3jkNtj0MKwewATldJPDcBsWKOGwonDqyWe3OJ84FL3vmkXJ4mDPVO7XZU/s1600/IMG_3319.JPG
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akimpa pole Baba mzazi wa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Marehemu John Gabriel Tupa Mzee Gabriel Tupa, baada ya mazishi yake yaliyofanyika leo Machi 29-2014 Wilayani Kilosa  Mkoani Morogoro.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg2PMH3owdBf7krOm2P4zFXb1KtptHWx3dIxIKZ3LH8DaWYND7uLZZ-AXdOobgwBZHH1V-573Zmt5acVQkd-1tBV7G8LKdKWMB5BUN_mQI5ai356SdKyRHptVLJtgJW9JJ4aXRZk5AYODwi/s1600/PG4A4975.JPG
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akimfariji  Mzee Gabriel Tupa baba mzazi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa  katika mazishi yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu  Kilosa achi 29, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh8ECkMzgIB8gpEnwD4Udmz0NbASCJkwEjmjlwDu7u2eRU01qOcIxeaNilNLtOzQDhYAZVaHSNJJLZs7tg-q0R4kVKeLyS73E-gPfUML57uo0bbbdC53a7R8ismigGY9tgamtCiiGTi1kAY/s1600/IMG_3299.JPG
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akimpa pole mjane wa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Marehemu John Gabriel Tupa Mama Katherine Msamati baada ya mazishi yake yaliyofanyika leo Machi 29-2014 Wilayani Kilosa  Mkoani Morogoro.

Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger