HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA
(MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA
SHUGHULI ZA MKUTANO WA 13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 09
NOVEMBA, 2013
I: UTANGULIZI
a) Masuala
ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Leo tunahitimisha shughuli za
Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge lako Tukufu.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa
kutufikisha salama siku ya leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Mkutano huu ulijumuisha kazi kubwa
zifuatazo:
Kwanza: Kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa kwa Mwaka 2014/2015;
Pili: Kujadili
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The
Written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2013];
Tatu: Kujadili Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba
wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013 [The GEPF Retirement Benefit Bill,
2013]; na
Nne: Kujadili
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional
Review Act) sura ya 83.
3. Nitumie nafasi hii kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa Bungeni
kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015.
Napenda kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri kama yalivyotolewa na
Waheshimiwa Wabunge yatazingatiwa na Serikali kila moja kwa uzito wake wakati
wa maandalizi ya Bajeti ya 2014/2015. Vilevile niwashukuru kwa kujadili na
kupitisha Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu.
b) Maswali
Mheshimiwa Spika,
4. Pamoja na kukamilisha kazi hizo
muhimu, pia katika Mkutano huu, jumla ya maswali 120 ya msingi na 305 ya
nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 6 ya msingi na 6 ya nyongeza
yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c)
Kauli za Mawaziri/Maazimio
Mheshimiwa Spika,
5.
Mkutano huu pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, Waheshimiwa Wabunge
walipata
fursa ya kujadili Azimio la Kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuhusu msimamo wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(d)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais,
Mheshimiwa Spika,
6. Katika Mkutano huu pia, Waheshimiwa
Wabunge walipata fursa ya kumsikiliza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Wananchi kupitia Bunge
lako Tukufu. Mtakubaliana nami kwamba
hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa nzito na yenye kuonesha umakini, umahiri na
busara ambazo ni sifa mojawapo za Rais wetu kati ya nyingi nzuri alizonazo.
Tunachotakiwa ni kutumia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa
Wananchi katika maeneo yetu ili nao waweze kuelewa hali halisi ya yanayotokea
katika Jumuiya yetu. Aidha, Hotuba ya Rais imegusa maeneo mengine ambayo sisi
Wabunge tunatakiwa kushirikiana na Wananchi katika kujipanga vizuri namna ya
kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza.
II:
UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI
YA MWAKA 2013/2014
(a)
Mwenendo wa Mapato na Matumizi ya
Serikali katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
7. Hotuba yangu kwa leo imejikita
zaidi kuelezea utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014 na maeneo
machache katika Sekta ya Kilimo na Nishati. Lakini kabla ya kuelezea mwenendo
wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014,
naomba kueleza kwa muhtasari kuhusu mwenendo wa baadhi ya viashiria muhimu vya
uchumi hususan Ukuaji wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa za awali
zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa Pato la
Halisi la Taifa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa
Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho
mwaka 2012. Sekta zilizoonesha kuwa na
Viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji
ambayo imekua kwa Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha Asilimia 14.6 na Sekta ya
Ujenzi Asilimia 8.7.
Mheshimiwa Spika,
8. Kwa upande wa Mfumuko wa Bei,
takwimu zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei imepungua kutoka Wastani wa
Asilimia 13.5 Mwezi Septemba, 2012 hadi Asilimia 6.1 Mwezi Septemba, 2013.
Kushuka kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa zaidi na upatikanaji wa chakula cha
kutosha ndani ya Nchi. Mwenendo huu mzuri wa viashiria vya uchumi jumla unatupa
matumaini makubwa kwamba jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa Uchumi
na kuleta Maendeleo endelevu ya Wananchi wetu zinaanza kuzaa matunda.
Mheshimiwa Spika,
9. Katika Robo ya Kwanza ya mwaka
2013/2014 kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba 2013, Mapato yote yaliyokusanywa na
Hazina yalifikia Shilingi Trilioni 3.08; sawa na Asilimia 85.7 ya makadirio ya
Shilingi Trilioni 3.59. Pamoja na mwenendo huo wa ukusanyaji mapato, changamoto
kubwa zinazokabili eneo la Mapato ya Serikali ni kuchelewa kuanza kwa wakati
kwa ukusanyaji wa Mapato katika baadhi ya vyanzo vya mapato. Changamoto
nyingine ni Miundombinu isiyokidhi mahitaji ya usafirishaji endelevu hasa reli ya
kati, bandari, usafiri wa Anga na barabara.
Miundombinu Bora ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa Uchumi na Kukuza
Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi kutokana na
kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Serikali inafanyia kazi changamoto hizo
ili kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika,
10. Kwa upande wa matumizi, hadi kufikia
mwezi Septemba 2013; matumizi yalifikia Shilingi Bilioni 3,806.5, sawa na
Asilimia 98.5 ya lengo la kutumia Shilingi Bilioni 3,854.2. Kati ya matumizi
hayo, Shilingi Bilioni 3,058 ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni 747.9
ni Matumizi ya Maendeleo. Katika kipindi
hiki, sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa
katika maeneo yenye kuleta ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha
miundombinu ya barabara, ambayo mgao wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5 za
Matumizi ya Kawaida na Maendeleo, Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2; Sekta
ya Nishati, Shilingi Bilioni 159.9; Sekta ya Kilimo Shilingi Bilioni 119.6 na
Sekta ya Maji Shilingi Bilioni 51.3. Vilevile, Serikali imelipa Mishahara ya
Watumishi wa Umma kwa wakati. Changamoto kubwa iliyopo kwenye matumizi ya
Serikali ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya matumizi yasiyowiana na mapato;
jambo ambalo linailazimu Serikali kukopa kutoka Mabenki ya Ndani. Serikali
itaendelea kuoanisha Matumizi na ukusanyaji wa Mapato, hasa yale ya ndani
pamoja na kuzingatia viwango vya Matumizi vilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha,
Serikali itaendelea kuweka msisitizo wa kuelekeza Matumizi kwenye vipaumbele
vilivyoainishwa katika Bajeti ya Serikali ambavyo ni vyanzo muhimu vya kuongeza
Mapato, Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.
III:
UTEKELEZAJI WA MFUMO MPYA WA
TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW - BRN)
(a)
Muundo wa Mfumo
Mheshimiwa Spika,
11. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa
Serikali ilianzisha Mfumo mpya wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa au Big Results Now (BRN) ili kuongeza ufanisi
katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mipango yetu ya
Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 -
2015/2016). Hatua hii ilichukuliwa baada
ya kuona namna Mfumo kama huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa, na hasa Nchi ya
Malaysia, kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi
kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo huo unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo
muhimu Kitaifa (National Key Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo
ni Nishati ya Umeme; Uchukuzi; Kilimo; Elimu; Maji na Ukusanyaji wa Mapato;
Mheshimiwa Spika,
12. Katika Hotuba yangu ya kuahirisha
Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6 Septemba 2013, nilitoa taarifa ya
awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu Mpya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai
hadi Septemba, 2013. Katika taarifa hiyo, nilieleza kuwa tumepiga hatua za
kuridhisha katika uundaji wa Mfumo wa
kuleta matokeo ya haraka, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi
wa juu wa Taasisi Maalum yaani "President’s Delivery Bureau (PDB)”
inayomsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi na
Programu zilizoainishwa. Hivi sasa zoezi
la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s Delivery Bureau” na
Vitengo vya Wizara vya Ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery Units (MDUs)
watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka kwenye Wizara na Taasisi
mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo za Kiserikali ambao
walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza. Ninapenda kutumia fursa
hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo hiki tangu kilipoundwa kwa
uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi hiki cha mwanzo na cha mpito;
Mheshimiwa Spika,
13. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu
kwamba hadi sasa vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita (6)
zinazosimamia utekelezaji chini ya Mfumo huu mpya vimeanzishwa na vinaandaa
Taarifa za utekelezaji za kila wiki na kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye
Chombo cha President’s Delivery Bureau. Aidha, Kamati Maalum za kusimamia
utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri husika zinakutana kila mwezi kujadili
mwenendo wa utekelezaji na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza
katika utekelezaji. Baraza la Kusimamia Mageuzi na Utekelezaji (Transformation
and Delivery Council – (TDC)) limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba, 2013.
Katika Kikao hicho, Baraza lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya
utekelezaji wa Mfumo mpya wa Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya
Kipaumbele katika Maeneo Sita ya Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na
hatua za awali za utekelezaji na lilitoa mwongozo stahiki wa hatua za
kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza litaendelea kukutana mara kwa mara ili
kutathmini na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa Mikakati iliyowekwa ya Mfumo huu
mpya;
(b)
Utekelezaji wa Mikakati katika
Maeneo Makuu Sita ya Matokeo Kitaifa;
Mheshimiwa Spika,
14. Utekelezaji wa mikakati katika maeneo
makuu sita ya matokeo kitaifa ulianza mara baada ya uchambuzi wa maabara
kukamilika. Mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika kila moja ya maeneo
yale sita, hasa ikizingatiwa kwamba Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika
utendaji Serikalini. Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa
fedha, kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013; baadhi ya matokeo
yaliyopatikana ni pamoja na yafuatayo:
(a)
Katika Sekta ya Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26 ya umwagiliaji
kwa Wakulima wadogo na pia imekarabati
maghala 26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika maeneo
yaliyopewa kipaumbele hasa katika eneo la SAGCOT.
(b)
Katika Sekta ya Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494
wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la
kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha, vipande
vya Bomba la Gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi wa Kilomita 243.8 za Bomba la
Gesi tayari vimewasili Nchini, na uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam umekamilika kwa Kilomita 124.3. Vilevile, Kilomita
447 za njia ya Bomba la Gesi zimesafishwa;
(c) Katika Sekta ya Elimu, Shule za msingi
5,916 zilipatiwa mitihani ya marejeo na mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo
la mwaka. Aidha, Mafunzo Kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika
Shule 1,325 sawa na Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;
(d)
Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini
wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya idadi ya Wananchi waishio
Vijijini ambao wanapata majisafi na salama kufikia takribani Milioni 15.9. Kasi
hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini imewezekana baada ya Wizara ya Maji
kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi husika kwa Sekretarieti za Mikoa na
Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo limewafanya Watendaji kuwajibika na
kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha, hatua zilizochukuliwa zimeiwezesha
Wizara ya Maji kuongeza ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma, ikiwemo
ujenzi na vifaa vyake, kutoka wastani wa siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za
sasa.
Mheshimiwa Spika,
15. Mafanikio haya na mengine mengi ambayo
sikuyataja hapa yameonyesha kuwa tukidhamiria, tunaweza kubadilisha kabisa
matokeo ya juhudi zetu na kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni Taifa la Kipato cha
Kati ifikapo mwaka 2025;
Mheshimiwa Spika,
16. Kufuatia mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi
Juni, 2013 kwa Watendaji wa Wizara husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala
wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana
na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili
kwa kina Taarifa za utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu.
Aidha, katika Vikao hivyo, nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote
Nchini kufanya yafuatayo:-
(a)
Kuchambua miradi iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo
ipo nje ya Mfumo wa “Tekeleza kwa
Matokeo Makubwa Sasa” kwa kutambua manufaa yanayotarajiwa baada ya kukamilika
na mahitaji halisi;
(b)
Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili kuweka mkazo katika miradi
itakayokamilika haraka na kuwa na manufaa makubwa kwa Wananchi; na,
(c)
Kuweka utaratibu wa Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa
miradi ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika,
17. Ninafurahi kutoa taarifa kuwa Wizara
na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza
kwa Matokeo Makubwa Sasa kwa hamasa kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya
kutekeleza majukumu yao katika Mfumo huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe
Vitengo vya kusimamia utekelezaji katika Ngazi ya Mkoa (Regional Delivery Units
(RDUs), sambamba na vile Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara ili utekelezaji
katika Maeneo Makuu ya Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na umakini stahiki.
Hatua hii inazingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama Elimu na Maji
ambayo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mchango mkubwa katika
utekelezaji yanapata msukumo wa kutosha. Kazi hii imeshaanza, na taarifa
zilizowasilishwa ni za kutia moyo sana.
Mheshishimiwa Spika,
18. Kwa kuzingatia mafanikio ya awali
yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara, Idara na Taasisi ambazo
bado hazijaingia katika Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa zisisubiri
hadi zitakapoingia rasmi bali zianze kujipanga na kutekeleza mipango, miradi na
program zao kwa kutumia mbinu ambazo zinatumika katika Mfumo huo pamoja na
Rasilimali fedha na Wataalam waliopo.
Msisitizo ni kwamba Wizara zote na Mikoa ijipange upya na kuongeza
ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya
maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa letu linafikia malengo ya maendeleo
tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Aidha, napenda kutumia
fursa hii kutoa wito kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuimarisha usimamizi wa Watendaji wao kwa kuzingatia taratibu za uwajibikaji
zilizowekwa chini ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi na tija ya utendaji
Serikalini pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya Kukuza Uchumi na
kuondoa umaskini;
IV:
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA
MAENDELEO YA TAIFA WA MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
19. Mwanzoni mwa Mkutano huu wa Bunge
Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda
kutumia fursa hii tena kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na michango
yao mizuri ambayo itatuwezesha kuboresha Mpango na Bajeti ya Mwaka ujao wa
Fedha 2014/2015. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.) pamoja na
Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta waliotoa maelezo fasaha ya ufafanuzi wa Hoja
zilizojitokeza wakati wa Mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa
kuzingatia michango mizuri na yenye tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na
Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya
Taifa wa mwaka 2014/2015, nami naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama
ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika,
20. Kama Waheshimiwa Wabunge
watakavyokumbuka katika majadiliano yaliyokuwa yanaendelea, moja ya jambo
ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya wingi wa
vipaumbele vya Taifa. Aidha, imeonekana
pia kuwa miradi ya maendeleo ni mingi sana kiasi kinachosababisha miradi hiyo kutotekelezeka kutokana na ufinyu
wa rasilimali fedha. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Vipaumbele
vilivyopendekezwa na Serikali vinategemeana na vinalenga kutanzua vikwazo vikuu
vya kiuchumi Nchini ili kufungua fursa za ukuaji wa uchumi wa Taifa na
kuharakisha maendeleo na ustawi wa Wananchi wa Tanzania. Pendekezo la Serikali
ni kuwa njia bora si kupunguza vipaumbele hivi sasa, bali ni kupanga vizuri
mtiririko wa utekelezaji wa miradi ndani ya kila kipengele ili kuongeza
jitihada za kuongeza Mapato, na kusimamia nidhamu ya matumizi.
Mheshimiwa Spika,
21. Kwa kuwa Mpango huu wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni wa kwanza unaojenga msingi wa mipango
mingine ya maendeleo ya miaka mitano
itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake itarahisisha
utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya msingi katika
mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane kwa karibu na
Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa katika ngazi zote inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa
mwanzo utekelezeke kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
22. Mjadala na Hoja nyingine zilijielekeza
katika changamoto za upatikanaji wa Ajira
kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012,
Asilimia 34.7 ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati ya miaka 15 -
35. Kundi hili la Vijana ndilo lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira cha
Asilimia 13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana hawa wamekuwa wakipata kazi
hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na Hoteli, ajira zao nyingi zimekuwa za
muda.
23. Katika kukabiliana na changamoto hii,
Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa Vijana itakayotekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitatu. Malengo ni kupatikana fursa za ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla
ya Miradi 10,000 ya Wahitimu wa Elimu ya Juu wapatao 30,000 kutoka Vyuo
mbalimbali ambao watatoa ajira za moja
kwa moja kwa wahitimu wengine 270,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 540,000.
Programu hii itajengea Vijana uwezo katika stadi za kazi; ujasiriamali; na
kuwapatia Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi; na kuwapatia Vijana
maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia kuelekeza fedha zaidi
katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa Programu hiyo. Aidha,
naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na
kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika,
24. Kilimo ni moja ya maeneo ya kipaumbele
katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili ndilo eneo kubwa kwa maana ya kuongeza
fursa za ajira na kipato kwa Wananchi wanaoishi Vijijini, kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi kwa namna ambayo ni shirikishi ili kupunguza umaskini. Hivyo, ili kujibu matatizo ya msingi ya
umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo
2014/2015 utatoa kipaumbele katika mambo muhimu yafuatayo:
(i) Utafiti wa kilimo cha mazao, hususan
katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi;
(ii) Kuimarisha huduma za ugani kwa kilimo,
mifugo na uvuvi na kuimarisha
upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa ajili ya kilimo;
(iii) Kuimarisha Ushirika wa Wakulima na
Wafugaji;
(iv)
Kuongeza fursa za mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni
pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014;
(v) Kuwezesha upatikanaji wa masoko ya
mazao ya kilimo, na mifugo;
(vi) Kujenga na kukarabati skimu za
umwagiliaji;
(vii) Upatikanaji wa ardhi kwa kilimo na
mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi;
na
(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi;
Mheshimiwa Spika,
25. Mpango wa Maendeleo huandaliwa katika
ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu ya Serikali ambazo ni:
Moja:
Vijiji na Mitaa;
Pili:
Kata;
Tatu:
Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri);
Nne:
Mikoa; na
Tano:
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali.
Mamlaka husika katika ngazi zote
zinatakiwa kuandaa Mipango yao kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama
yalivyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015.
Mipango lazima ilenge katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka
hususan katika kuchochea maendeleo ya maeneo mengine na Programu nyingine
katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Katika kila ngazi, Wadau wengine kama
vile Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika
wa Maendeleo washirikishwe kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi
na Wakala wa Serikali ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango Wiki ya Nne ya mwezi Januari, Mwaka 2014.
Katika ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji
uanze katika ngazi ya Kijiji na Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye
Mkoa. Mpango uliopitishwa na Mkoa uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari,
2014. Mpango wa Maendeleo wa Taifa
utajadiliwa na Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni, 2014 na utekelezaji wake
utaanza Mwezi Julai 2014 hadi Juni 2015;
Mheshimiwa Spika,
26. Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika utayarishaji wa Mipango ya Maendeleo ya
Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa fedha 2014/2015. Hivyo, nawaomba
Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa hapa Bungeni kutoa ufafanuzi
kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika Halmashauri zao wakati wa kujadili
Mipango yao. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Mamlaka za Serikali za
Mitaa kuainisha vipaumbele vinavyolenga katika maeneo yenye kuleta matokeo
makubwa na ya haraka ya Kiuchumi na Kijamii; na pia yenye kuchochea maendeleo
ya maeneo mengine. Vilevile, vipaumbele vya Halmashauri vilenge kufungulia
fursa za ajira, kuongeza mapato ya ndani na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi
katika maeneo yao.
V: SEKTA YA KILIMO
a) Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
27. Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa
Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba 2013 ni ya kuridhisha kufuatia mavuno
mazuri ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambapo mazao yake yanaendelea kuingia
sokoni kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya awali iliyofanyika
mwezi Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika
Msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani 14,383,845 za chakula zikiwemo Tani
7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka. Kiasi
hicho cha chakula kilichozalishwa ni ongezeko la Tani 2,234,726 za chakula,
ikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2013/2014 ya Tani 12,149,120.
Kiwango hicho kinajumuisha Tani 354,015 za mahindi na Tani 466,821 za mchele.
Hivyo napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kuwa
tutakuwa na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.
Mheshimiwa Spika,
28. Vilevile, tathmini hiyo inaonesha
kuwa, pamoja na kuwepo kwa chakula cha kutosha na cha ziada, Halmashauri 61
katika Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga,
Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora
zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.
29. Natoa wito kwa Halmashauri
zinazohusika katika Mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata
chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kuwa kinafika
mapema kwenye maeneo yao kabla Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika.
(b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
30. Kutokana na hali ya upatikanaji wa
chakula kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika
Soko Nchini zimeendelea kushuka. Kwa mfano, bei ya mahindi ilishuka kutoka
Shilingi 774.30 kwa kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi 535.40 kwa Kilo
mwezi Septemba 2013. Kwa upande wa mchele, bei kwa kilo moja imeshuka kutoka
Shilingi 1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi
Septemba 2013, na bei ya mchele imeshuka zaidi hadi kufikia Shilingi 1,146.70
katika mwezi Oktoba, 2013.
(c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula
ya Taifa
Mheshimiwa Spika,
31. Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula imepanga kununua Tani 250,000 za nafaka katika msimu wa
2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2013, Wakala alikuwa amekwishanunua
kiasi cha Tani 218,412 za nafaka sawa na Asilimia 87.37 ya lengo lililowekwa
ambapo Tani 217,919 kati ya hizo ni za Mahindi na Tani 493 ni za mtama. Aidha,
hadi kufikia tarehe 23 Oktoba 2013, maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula yalikuwa na jumla ya Tani 232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani 232,419
ni za mahindi na Tani 493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka kinajumuisha
albaki ya Tani 25,452 za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,
32. Serikali inaendelea na tathmini ya
kina ya hali ya chakula na lishe katika Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na
hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa
chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa
mara nyingine tena kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa
walioko katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa
mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula wajipange
vizuri kuhamisha Chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo
yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara taarifa ya upungufu itakapotolewa.
Mheshimiwa Spika,
33. Pamoja na juhudi za Serikali za
kuhakikisha kwamba kuna chakula cha kutosha, natambua Changamoto zilizopo
katika ununuzi wa Chakula kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula.
Natambua kuwepo kwa madeni yanayotukabili kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya
Wakala yaani NRFA. Hata hivyo, Mikoa
inayohusika na madeni hayo ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa
na Tanga. Serikali itahakikisha deni hilo hilo linalipwa ndani ya mwaka huu wa
fedha 2013/2014.
(d) Mpango wa Pembejeo za Ruzuku
Mheshimiwa Spika,
34. Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 12
wa Bunge, katika msimu wa 2013/2014 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni
112.564 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea kuhusu
utaratibu mpya wa kutoa ruzuku utakaohusisha uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na
Asilimia 20 mikopo. Ili kuhakikisha
Mfumo huu mpya unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa,
Serikali imetoa mafunzo ya utoaji pembejeo kwa njia ya mikopo kwa Washauri wa
Kilimo wa Mikoa, Maafisa Ushirika wa Mikoa na Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya
kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na
Manyara; na Awamu ya Pili inahusu Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Iringa.
Aidha, uchambuzi wa takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima
watakaokopeshwa pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika Mikoa ya
Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara. Takwimu zinaonesha kuna SACCOS 214, AMCOS 163
na Vikundi vingine 51 vyenye Wakulima 88,290 watakopeshwa pembejeo za Kilimo.
Natoa Wito kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendeleza mafunzo haya
kwa Mikoa iliyobaki.
(e) Hali ya Usambazaji wa Vocha za
Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
35. Kuhusu hali ya Usambazaji wa Vocha za
Pembejeo katika Msimu wa 2013/2014 napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba,
jumla ya Vocha 2,796,300 kwa ajili ya Kaya 932,100 zikiwemo Vocha 932,100 za
mbolea ya kupandia, 932,100 za mbolea ya kukuzia, Vocha 441,100 za mbegu za
mahindi chotara; Vocha 432,000 za mahindi ya OPV na Vocha 60,000 za mbegu za mpunga
zilisambazwa katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito kwa Viongozi wa Mikoa na
Wilaya kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine kuhakikisha
kuwa Wananchi wanapata na wanatumia Vocha hizi kupata pembejeo kama
ilivyokusudiwa. Aidha, tushirikiane kuhakikisha kuwa wale watakaokwenda kinyume
na utaratibu huu wa usambazaji wa Vocha hizo wanashughulikiwa kwa mujibu wa
Sheria.
(f) Changamoto za Mbolea ya Minjingu
Mheshimiwa Spika,
36. Juhudi za Serikali katika kuhakikisha
upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko dhahiri.
Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji ya mbolea, kilio kikubwa
cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati.
Aidha, wapo Wananchi wanaolalamikia mbolea ya Minjingu Mazao ambayo ni
kweli hapo awali ilikuwa na matatizo.
Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuongezewa
virutubisho.
Mheshimiwa Spika,
37. Mbolea ya Minjingu ya awali ilikuwa na
virutubisho vya udongo viwili tu vya Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya Minjingu
Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vinne zaidi na kufanya virutubisho
hivyo kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti, Naitrojeni, Salfa, Boroni na Zinki.
38. Kwa msingi huo, Mbolea ya Minjingu
mazao inaweza kutumika katika aina mbalimbali za udongo tofauti na ilivyokuwa
awali. Aidha, Mbolea ya Minjingu Mazao ni ya chengachenga (granulated) tofauti
na ya awali ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga (dust) ambapo pengine matumizi
yake hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya kuboreshwa, kwa sasa Mbolea hii ya
Minjingu inatumika kwa mazao mengi hususan mahindi, mpunga na alizeti katika
sehemu mbalimbali na aina mbalimbali za udongo.
Mheshimiwa Spika
39. Mkulima anahitaji kutumia mifuko
miwili ya mbolea ya Minjingu Mazao ya kilo 50 kila mmoja kwa wakati mmoja
ikilinganishwa na mfuko mmoja wa kilo 50 wa mbolea ya DAP. Hata hivyo, ukilinganisha na mbolea ya DAP,
mkulima anayetumia Minjingu Mazao anawezesha shamba lake kupata virutubisho
zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu Mazao ni nafuu ikilinganishwa na Mbolea ya
DAP.
40. Bei ya mbolea ya Minjingu Mazao kwa mfuko mmoja ni Shilingi
32,500/= hivyo kwa mifuko miwili ni Shilingi 65,000 katika Wilaya zote Nchini
ikilinganishwa na bei ya wastani ya Shilingi 75,000/= ya mfuko mmoja wa DAP.
Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika kupandia, lazima mkulima
aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina virutubisho vingi vya Naitrogeni kama CAN au UREA.
41. Majaribio ya kutumia Mbolea ya
Minjingu yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka 2006 ikiwa katika hali ya
unga. Mwaka 2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuiweka katika hali ya chenga
chenga (granulation) ingawa virutubisho havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea
kutumika katika hali hiyo hadi mwaka 2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo
iliboreshwa kwa kuongezea virutubisho ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki
(validation) iliingizwa Sokoni mwaka
2012.
42. Kwa sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao
inatumika katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma
na Morogoro. Aidha, kuna mikoa mingine ambako mbolea hii imepelekwa pamoja na
mbolea nyingine kwa ajili ya Wakulima wenyewe kufanya maamuzi ya kuchagua.
Mheshimiwa Spika
43. Matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao
katika mwaka 2012/2013 yamewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga
na alizeti kwa ekari hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Changamoto
kubwa ni elimu juu ya matumizi sahihi ya Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.
44. Katika kutatua changamoto hii, Wizara
inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu kuendesha mashamba
darasa katika Wilaya mbalimbali Nchini.
Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti katika maeneno mbalimbali ya Nchi ili
kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo katika aina mbalimbali za udongo (site
specific validation trials).
45. Changamoto zinazohusiana na Mbolea ya
Minjingu katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa kwa namna yake. Kitendo hicho ni
cha udanganyifu kwani Mbolea ya aina nyingine ni bei kubwa ikilinganishwa na ya
Minjingu Mazao. Kutokana na kitendo hicho kuwa kinyume na Sheria ya Mbolea ya
2009, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa
Wilaya ya Mbozi ilimkamata Wakala husika na kumchukulia hatua za kisheria.
Naagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuchunguza mbolea inayopelekwa katika
maeneo yao isije ikachakachuliwa.
Mheshimiwa Spika,
46. Kwa kuzingatia Changamoto
zilizojitokeza katika matumizi ya mbolea ya Minjingu katika maeneo mbalimbali
Nchini Serikali itaendelea kuzitafutia ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a) Kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu namna
bora ya kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa
kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa
mbolea hiyo. Vilevile, kuwaelimisha Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu
Mazao ikilinganishwa na Mbolea za aina nyingine hasa kutokana na virutubisho
vilivyoongezwa katika mbolea.
(b) Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
imeagizwa kufuatilia na kufanya uchunguzi wa madai ya Wakulima kuhusu
changamoto za matumizi ya mbolea ya Minjingu Mazao hasa katika Wilaya ya Mbozi
na sehemu nyingine zenye matatizo ya matumizi ya mbolea hiyo Nchini.
(c) Naomba kuiagiza Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika kuendelea kushirikiana na Wadau kufanya utafiti katika
maeneo mbalimbali Nchini. Kutokana na utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa
Wakulima wote Nchini kuhusu njia sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao
katika aina mbalimbali za udongo na mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza
tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa eneo. Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe mwongozo
kuhusu nini kifanyike kwa sasa wakati hatua za utafiti na uchunguzi wa matumizi
sahihi ya Mbolea hiyo zinaendelea.
(g) Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya
Biashara
Mheshimiwa Spika,
47. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa
na Changamoto mbalimbali za uzalishaji na ununuzi wa baadhi ya mazao ya
biashara hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha zao la Pamba, Korosho, Tumbaku na
Kahawa. Kwa kuzingatia ufinyu wa muda, leo naomba mniruhusu nizungumzie kidogo
kuhusu kilimo cha mazao mawili ya Pamba na Korosho.
(h) Uzalishaji na Ununuzi wa Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
48. Serikali inaendelea na jitihada za
kuhakikisha kuwa Wakulima wa Pamba wanazalisha kwa tija kwa kutumia mbegu bora, utumiaji wa
pembejeo (Viuadudu na Mbegu), kutoa huduma za ugani kupitia Maafisa wa Kilimo
katika Halmashauri za Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa
kushirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi.
49.
Katika kilimo hiki cha Pamba,
Zana za kilimo zinazotumika kwa sasa ni majembe ya kukokotwa na wanyama kazi
kwa ajili ya kulima nah ii ni dhahiri haiwezi kuongeza tija. Ttahakikisha
tunatumia Zana za Kisasa.
(i) Mkakati wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba
50. Serikali pia inaendelea kuhakikisha
kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini kwa kuhamasisha uwekezaji katika
ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo. Uwekezaji mpya unafanyika kwa kujenga
kiwanda cha nyuzi na nguo cha Dahong Mkoani Shinyanga na pia Mradi mkubwa wa
kuzalisha pamba, kuchambua, kutengeneza nyuzi, kutengeneza vitambaa na nguo
unaotarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya
Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni. Kwa sasa mradi huo uko katika hatua
ya umilikishwaji wa Ardhi.
51. Vilevile, Serikali imeanzisha mafunzo
ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo. Pia tumeanzisha kozi
ya ubunifu wa mitindo katika mitaala ya VETA na Mafunzo ya Shahada ya uzamili
katika “Textile” katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa
kuna watalaamu wa kutosha katika mchakato wa kuongeza thamani ya pamba.
(j) Tofauti za ubora wa mbegu za pamba
manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52. Sina shaka Watanzania wameshasikia
kuwa kwa sasa tunazo aina mbili za mbegu za Pamba zinazotumika hapa
Nchini. Tunayo mbegu yetu ya asili ya
Pamba Manyoya na Mbegu mpya na ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya
(De-linted). Aina hizi zinatofautiana
sana kwa ubora na bei. Mbegu ya manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50
wakati ile ya De –linted ni zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika
nyingi kwa eneo (kilo 25 kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6 tu kwa Ekari,
sawa na Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo. Mbegu ya
manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya kilo 250 na 300 kwa Ekari)
ikilinganishwa ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 – 1200 kwa Ekari.
Mbegu ya manyoya ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33) ikilinganishwa
na mbegu De-linted ambayo uwiano wake ni
Asilimia 36.
(k) Jitihada za Wizara kupunguza bei ya
mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53. Ili kuwawezesha Wakulima kutumia mbegu
bora (de-linted) Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi Billioni 4.8 ili kufanya
mbegu hiyo ipatikane kwa Shilingi 600 kwa kilo kwa mkulima badala ya Shilingi
1,200 kwa kilo iliyotumika mwaka 2012/2013.
54. Serikali pia inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kutoa elimu kwa wakulima wa pamba kuhusu mbegu bora. Kwa mfano,
Viongozi wa maeneo yanayolima pamba (Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi
ya Madiwani) wamepelekwa katika kiwanda
cha kuchakata mbegu bora za Pamba cha
Kampuni ya Quton ili kupata maelezo na
kujionea hali ya utendaji wa mbegu bora katika kilimo.
55. Kupitia programu ya kuendeleza zao la
pamba wakulima wawezeshaji (Lead Farmers) 3000 wa vikundi vya Kilimo cha
Mkataba wanaendelea kupewa mafunzo ya kilimo bora na matumizi ya mbegu bora ili
watumike kupeleka elimu hii kwa wakulima wenzao.
Mheshimiwa Spika,
56. Katika msimu huu wa Kilimo wa 2013/14,
Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwa lengo la
kuleta ufanisi katika Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii inahusisha pia kutoa elimu ya kutosha na kushirikisha kwa karibu Wadau katika
kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye utaratibu mzima wa kilimo
hicho ambacho kina manufaa makubwa iwapo kitaeleweka na kutekelezwa vyema kwa
misingi ya haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa hayo ni:
(i) Uhakika wa upatikanaji wa pembejeo
kwa mkulima kwa mkopo.
(ii) Kuongeza tija kutokana na kupata
pembejeo na huduma za ugani.
(iii) Kuongeza ubora wa pamba kutokana na matumizi makubwa ya pembejeo na huduma
za ugani pamoja na vikundi kutumika kama
Mawakala wa kununua Pamba ya wanachama wake hivyo kusimamia ubora
(iv)
Uhakika wa soko la pamba ya
mkulima
(v)
Kupunguza wizi kupitia mizani ya mawakala
(vi)
Wakulima kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii)
Kujenga na kuimarisha mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.
(l) Elimu ya kilimo cha mkataba kwa
wakulima
Mheshimiwa Spika,
57. Kupitia programu ya kuendeleza zao la
pamba, wakulima Wawezeshaji zaidi ya 3,000 wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo
cha Mkataba wanao tumika kupeleka elimu hii kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa
Halmashauri wapatao 560 wameshapata mafunzo haya. Chini ya Mpango huu kila mgani anaweza
kuhudumia vikundi hadi 20.
58. Napenda kuwaagiza Viongozi na
Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na faida ya mbegu bora za
De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa Wakulima wa Pamba Nchini. Aidha,
mashamba darasa yatumike ipasavyo kuonesha tija inayotokana na aina hiyo
ya mbegu za Pamba inapolinganishwa na mbegu zenye manyoya. Vilevile, Viongozi na Wataalamu wa Kilimo
waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na Watanzania kuwa utaratibu mpya wa
Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi na makubwa. Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na
Kilimo cha Mkataba bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia
mashamba darasa. Wale watakaoshawishika
kuingia katika utaratibu huu wasaidiwe kwa kila hali ili wanufaike na kilimo
hicho huku wakisaidia kutoa elimu kwa Wakulima wengine ili wajiunge na aina hii
ya kilimo. Ni matumaini yangu ndani ya muda mfupi Wakulima watafahamu faida ya
kilimo cha mkataba.
(m) Zao
la Korosho
Mheshimiwa Spika,
59. Kuhusu Zao la Korosho, azma ya
Serikali ni kuimarisha Viwanda vya Korosho na kufufua vile vilivyopobinafsishwa
ili viweze kusaidia kukuza Soko kwa wakulima wa Korosho. Ili kutekeleza azma
hiyo, Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa Wawekezaji wengi katika
Viwanda vya Korosho vilivyobinafsishwa wameshindwa kutekeleza Mikataba ya
Ubinafsishaji wa viwanda hivyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu
wa fedha za uendeshaji, ukosefu wa nishati ya uhakika na Viwanda kutumia
teknolojia zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mali za
Mashirika ya Umma (CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa mapendekezo ya hatua
za kuchukua dhidi ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda hivyo. Dhamira
ya Serikali ni kwamba Mwekezaji ambaye ameshindwa kuendeleza kiwanda
alichonunua kwa kuzingatia Makubaliano ya ununuzi na Serikali, mali hiyo
irudishwe Serikalini na ifanyiwe tathmini na itangazwe upya ili kupata
Wawekezaji mahiri na wenye nia thabiti ya kuendeleza Viwanda husika.
Mheshimiwa Spika,
60. Sambamba na hatua hiyo, Bodi ya
Korosho Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa miaka mitatu kuanzia mwaka
2012/2013 ambao umelenga kuwasaidia wabanguaji wadogo na wa kati kuendesha
shughuli za ubanguaji kwa ufanisi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kubangulia,
na kuwatafutia masoko ya ndani, masoko ya kanda na masoko ya nje;
61. Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba,
Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho
Tanzania umetenga fedha kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Mikoa ya
Ruvuma, Mtwara, na Pwani kwa ajili ya kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati
kumalizia baadhi ya hatua za ubanguaji katika viwanda hivyo kwa ajili ya
kukidhi matakwa ya masoko makubwa ya korosho duniani.
Mheshimiwa Spika,
62. Ili kuboresha kilimo cha Korosho, katika
mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya madawa kutoa huduma za
ugani na kuhamasisha wakulima wahudumie mikorosho na kupuliza madawa mapema.
Mheshimiwa Spika,
63. Kuhusu ununuzi wa Korosho, katika
msimu huu wa 2013/2014 ununuzi wa Korosho utaendelea kwa kutumia mfumo wa
Stakabadhi za mazao Ghalani. Ukusanyaji wa Korosho kutoka kwa wakulima umeanza
katika maeneo mbalimbali Nchini. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mtwara, mnada wa
kwanza wa Korosho ulianza tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo ulihusisha Vyama vya
Msingi vya Mkoa wa Mtwara. Korosho zote zilizokuwa zimekusanywa na kutangazwa
katika kila mnada zilinunuliwa. Bei ya Korosho katika Mnada wa kwanza ilikuwa
kati ya Shilingi 1,402/= na 1,520/= kwa
kilo ikilinganishwa na bei dira ya Shilingi 1,000/= kwa kilo. Mnada uliofuatia
bei ziliongezeka na kuwa kati ya Shilingi 1,481/= na 1,570/= kwa kilo.
Mheshimiwa Spika,
64. Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya
Msingi vilivyobaki chini ya ILULU vilifanya Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba,
2013 ambapo jumla ya Tani 783.593 ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya kutoka Wilaya
ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka usimamizi wa Chama
Kikuu cha ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata Kamati
itakayowasimamia zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada yake
katika Wilaya ya Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.
Mheshimiwa Spika,
65. Kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, bado
haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi za kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka
Benki ya NMB inaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya
TAMCU kupata mkopo msimu huu kwani deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na
Benki hiyo ya NMB limelipwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
66. Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano
wa Vyama vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Coast Region Cooperative Union
(CORECU) kupata Mkopo ni mdogo kutokana na kudaiwa fedha nyingi zaidi ya
Shilingi Bilioni 7 za msimu wa mwaka 2010/2011. Serikali imefanya Ukaguzi
Maalum katika Vyama hivyo na kubaini kwamba madeni hayo kwa kiwango kikubwa
yamesababishwa na ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji wa Vyama hivyo. Hivyo,
kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za kisheria zimechukuliwa
ikiwa ni pamoja na kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia hasara hiyo. Kwa
upande mwingine, Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye dhamana
imezitupilia mbali rufaa hizo zote 434, na kuwataka Wahusika walipe kiasi cha fedha
kinachodaiwa na Vyama vyao. Kutokana na hali hiyo, Wakulima wa Mkoa wa Pwani
wanashauriwa kupeleka mavuno ya Korosho katika maghala yaliyoteuliwa. Minada ya
Korosho itafanyika katika maghala hayo na wakulima watalipwa mara moja baada ya
minada kufanyika.
Mheshimiwa Spika,
67. Kutokana na jitihada za Serikali
zinazoendelea natoa wito kwa Bodi ya Korosho na Wakuu wa Mikoa husika kuendelea
kusimamia kikamilifu taratibu wa ununuzi wa Korosho ili kuhakikisha kwamba
Wakulima wanauza Korosho zao walizovuna na kulipwa malipo yao halali kwa
wakati.
(n) Hali ya mwenendo wa Mvua za vuli
mwaka 2013 na athari kwa mazao ya vuli
Mheshimiwa Spika,
68. Taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa hali
ya hewa hususan mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2013 iliyotolewa na
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini inaonesha kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa
chini ya wastani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa
Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya maeneo katika mikoa ya Mwanza,
Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja na kwamba mvua za msimu wa vuli
zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo yalitarajiwa kupata mvua za vuli,
mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa kuridhisha.
(o) Athari za mvua za vuli
zinazonyesha chini ya Wastani
Mheshimiwa Spika,
69.
Kutokana na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini ya awali iliyofanyika
katika maeneo yaliyotarajiwa kupata mvua za vuli inaonesha kuwa:
i.
Hali ya mazao hasa katika Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani
Kaskazini si ya kuridhisha,
ii.
Mategemeo ya mavuno ya vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo
ya ukanda wa Ziwa Viktoria hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo
yamepata mvua za wastani hadi chini ya wastani,
iii.
Mchango wa mavuno ya vuli ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula
kinachozalishwa katika maeneo yanayopata mvua hizo au Asilimia 18 Kitaifa
hauwezi kufikiwa katika hali hii ya mvua.
iv.
Hali hii inaashiria kuwa kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo
hayo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika,
70. Kutokana na hali hii, natoa wito kwa
Wakulima katika maeneo haya kuzingatia ushauri wa kupanda mazao yanayostahimili
ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika
Halmashauri husika wasimamie suala hili kwa ukamilifu; ili kuepusha upungufu wa
Chakula unaotarajiwa.
VI:
NISHATI
(a)
Kuongezeka kwa upatikanaji wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali
iliyofikiwa
Mheshimiwa Spika,
71. Wakati wa Kuhitimisha Mkutano wa 12 wa
Bunge nilieleza Mikakati ya Serikali katika kueneza umeme Vijijini na matarajio
ya baadaye. Napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tumeweza kupiga hatua
katika baadhi ya maeneo katika kuelekea kwenye malengo tuliyojiwekea. Tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
ulitangaza zabuni mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya kuwapata Wakandarasi wa
kupeleka umeme Vijijini na kujenga vituo vya kupoozea umeme. Baada ya tathmini
kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme Vijijini zilipata Wakandarasi. Mikoa
ambayo ilipata Wakandarasi
katika awamu hiyo
ni pamoja na Arusha,
Dodoma, Iringa, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe,
Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora. Aidha Wakandarasi
kwa ajili ya
ujenzi wa vituo
vya kupozea umeme vya msongo wa
Kilovoti 11 na 33 vya Ngara, Kibondo, Kasulu, Kigoma, Tunduru
na Mbinga walipatikana.
Kwa sasa Wakala unaendelea na kulipa malipo ya awali (advance payments)
na Wakandarasi wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza kazi. Miradi hii yenye thamani ya Shilingi Bilioni
430.82 inatarajiwa kukamilika mwezi Juni,
2015.
Mheshimiwa Spika,
72. Mwezi
Mei, 2013 zabuni nyingine 10 ya
Miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 450 zilitangazwa kwa
ajili yakuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini
katika Mikoa ya Geita,
Kagera, Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa na Tanga. Kwa sasa tathmini ya zabuni
hizo inaendelea. Inatarajiwa kwamba Wakandarasi kutokana na Tathmini hiyo
watajulikana ifikapo tarehe 15 Novemba, 2013.
(b) Suala la Fidia, Sera; na
Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:
Mheshimiwa Spika
73. Ili kuharakisha maendeleo ya
upatikanaji wa Nishati Vijijini, suala la
Wananchi kuchangia nguvu kazi na kutoa njia na maeneo ya kupitisha nyaya
za umeme bila fidia
pale inapowezekana limekuwa
likisititizwa na Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti. Upo ukweli kwamba,
Miradi mingi imechelewa kutekelezwa kutokana na Wananchi kudai fidia ya miti na
mazao ya msimu yanayokutwa kwenye njia ya umeme. Kwa mfano miradi ya Awamu ya Kwanza katika
Mkoa wa Pwani imechelewa kuanza na kukamilishwa kutokana na Wananchi kudai
fidia ilipwe kwanza ndio ujenzi uendelee. Pia, kwa sasa ujenzi umesimama katika
maeneo ya Bungu-Nyamisati na Kisiwa cha Mafia kutokana na Wananchi kudai fidia
kwanza.
Mheshimiwa Spika,
74. Ni kweli kwamba kulingana na Sheria
zilizopo kama katika njia ya kupitisha umeme yapo mazao yanayostahili kulipwa
fidia. Hata hivyo kutokana na bajeti finyu Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa
kutoa fidia inayohitajika na kuona ni bora wale wanaojitolea maeneo yao
wapelekewe umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa ajili ya fidia. Serikali
inatoa rai kwa Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea maeneo yao ili
waweze kupata huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge
tushirikiane katika kuwahamasisha Wananchi katika maeneo yetu kuhusu umuhimu wa
kupata umeme mapema kwa maendeleo ya maeneo yetu.
(c) Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la
Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam
Mheshimiwa Spika,
75. Shughuli za ujenzi wa Bomba la Gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri. Mpaka sasa usafishaji wa
njia ya kulaza bomba unaendelea na tayari Kilometa 484.17 kati ya Kilometa 517
zimekamilika. Aidha jumla ya mabomba 20,491 yanayotosheleza kulazwa umbali wa
Kilometa 243.8 yamekwishawasili Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga
mabomba katika mstari mmoja kwenye mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa kuchomelea
inaendelea na hadi sasa Kilometa 124.3 zimeshaunganishwa. Kazi zinazoendelea ni
ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi katika maeneo ya Songo Songo na Madimba,
pamoja na maandalizi ya ujenzi wa mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia.
Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa Mradi huu
muhimu kwa Taifa letu.
76. Aidha, katika kuhakikisha kwamba
miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa katika Nchi yetu, ninayo furaha
kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ilipitisha Sera ya Gesi Asilia
tangu tarehe 10 Oktoba 2013, Utaratibu wa kuichapisha sera hiyo katika lugha ya
Kiswahili na Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Nishati
na Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Sera ya
Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni matumaini yangu kwamba
vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia itaimarika.
VII:
MIFUGO
(a) Operesheni Ondoa
Mifugo Katika Maeneo Mbalimbali Nchini
Mheshimiwa Spika,
77. Kwa muda mrefu sasa maeneo mbalimbali
hapa Nchini yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayotokana na matumizi ya Ardhi
hususan kwa Wafugaji wanaohama kutoka maeneo yaliyokatazwa kisheria kwenda eneo
lingine pasipo na maandalizi ya kutosha ya kuwapokea. Utafiti unaonesha kuwa,
migogoro ya ardhi hapa Nchini ina sura nne:
Moja:
Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
Pili:
Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,
Tatu:
Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na
Nne:
Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali
inayotokana na migongano ya kimaslahi.
Mheshimiwa Spika,
78. Kuna ukweli kwamba, kuongezeka kwa
idadi ya Watu na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi kutaendelea kuongeza kasi na
vipaumbele katika kugawa maeneo yaliyoko wazi. Hali hii imeanza kuonekana
katika maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea kupungua siku hadi siku. Aidha,
shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na matumizi mengine ikiwa ni pamoja na
kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na ongezeko la idadi ya watu kumeendelea
kupunguza eneo la malisho.
Mheshimiwa Spika,
79.
Kuna ukweli pia kwamba,
mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo ya Nchi kwa
ajili ya kutafuta malisho na maji kumeendelea kuchangia migogoro mingi kati ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Kati ya mwaka 2005 na sasa, tumeshuhudia
uhamiaji wa mifugo kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwenda katika
Mikoa ya Kusini na Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo licha ya kusababisha
migogoro kati ya watumiaji wengine pia imesababisha uharibifu mkubwa wa
mazingira kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za Taifa. Baadhi ya
maeneo hayo ni pamoja na hifadhi za Wanyama pori za Burigi, Maswa na Meatu,
Bonde la Usangu na Bonde la Kilombero.
Mheshimiwa Spika,
80. Ni matumaini yangu kwamba, maadam
suala hili limepewa umuhimu na Bunge lako Tukufu na hivyo kuunda Kamati ya
kufuatilia migogoro hii, ni dhahiri tutapata ufumbuzi wa kudumu katika tatizo
hili. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaotoka
katika maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na Wakulima kutoa
ushirikiano katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa ili kulisaidia
Taifa katika kutatua migogoro hii.
VIII: HALI YA ULINZI NA
USALAMA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
81. Kwa ujumla hali ya Ulinzi na Usalama
Nchini imeendelea kuwa shwari, isipokuwa katika maeneo machache ambako
kulijitokeza vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa vikundi vya uhalifu na ujambazi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea
kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiusalama ikiwemo ugaidi. Tukio
lililotokea Nchini Kenya hivi karibuni na matukio ya kukamatwa kwa Vijana 12
kule Mtwara na lile lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo zaidi ya
watuhumiwa 46 wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanaashiria kwamba
ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea katika Nchi yoyote.
Mheshimiwa Spika
82. Katika kuhakikisha kuwa amani na
utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali imejipanga katika maeneo hayo kama
ifuatavyo:
(i)
Kuhakikisha Vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na
Vitongoji vinafanyika mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali
za Mitaa katika kila Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili na
kubaini kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
(ii)
Kufufua mpango wa Daftari la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji
kwa Tanzania Bara na Zanzibar ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji
ajue Watu wanaoishi katika himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka tatizo la
wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu. Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za
Serikali za Mitaa na Vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa Halmashauri wa
kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa
kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili
kuimarisha usalama katika Halmashauri
husika.
(iii)
Kuhimiza wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi
shirikishi/ulinzi jirani vilivyo kwenye maeneo jirani na biashara zao kama
sehemu ya kuimarisha usalama wa maeneo yao ya biashara. Pia, kwa wafanyabishara
wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya Watu wengi wanaagizwa kufunga “CCTV
Camera” na kuziunganisha kimtandao na “Control Room” ya Polisi ili kutoa msaada
wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu wowote utakaojitokeza.
(iv)
Kuendelea kuunda Zonal Task Force za Jeshi la Polisi katika kila
Tarafa/Jimbo ili kukusanya taarifa za uhalifu na kufanya operesheni za kuzuia
uhalifu katika kila Kata au Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa kufanya
hiovyo tutaokoa maisha ya watu wengi.
(v)
Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na
kupambana na uhalifu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari, mihadhara,
mikutano, maonesho na usambazaji wa machapisho na vipeperushi.
Mheshimiwa Spika,
83. Jukumu la kuhakikisha Ulinzi na
Usalama katika Nchi yetu ni letu sote.
Kila Mwananchi popote alipo anawajibika kushiriki kwa vitendo kwa
kubaini vitendo vyovyote vya uhalifu katika sehemu za kazi, biashara na maeneo
tunamoishi. Wito wangu kwa Waheshimiwa
Wabunge wote, ni kuwaomba tuwahimize Wananchi kushiriki kikamilifu katika
kuhakikisha Nchi yetu inadumu katika hali ya Amani na Utulivu.
IX: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
84. Kwa kuhitimisha, naomba nitumie nafasi
hii ya mwisho kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee
nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza
vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge
kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge
kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru
Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na
Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na
huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa
Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na
maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri
waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
85. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari
njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Baada ya
kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
tarehe 3 Desemba, 2013 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 14
kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
86. Naomba kutoa hoja.

Post a Comment