MWIGAMBA AZIDI KUIBUA MAZITO
* AMTOLEA
UVIVUMBOWE,ASISITIZA MABADILIKO
Pamela Mollel na
Goodluck Hongo
Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Arusha, Bw. Samson Mwigamba,
amesema kutokana na uadilifu wake na mapenzi mema aliyonayo katika chama,
ameamua kuachia madaraka kwa muda ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Bw. Mwigamba aliyasema hayo Mjini Arusha jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari pamoja na kutoa tuhuma nzito dhidi ya
viongozi wakuu wa chama hicho akiwataka waondoke madarakani.
Alisema viongozi hao wameonesha udhaifu katika mipango ya
chama hicho kutaka kushika dola na kusisitiza kuwa, Mwenyekiti wa chama hicho
Taifa, Bw. Freeman Mbowe, ameshindwa kazi ya kukiongoza chama hicho.
“Chama kimeshindwa katika mambo mbalimbali zikiwemo
operesheni zake kutokana na uwezo wa Mbowe kufikia mwisho, kitendo cha mimi
kutoa maoni ya kutaka Mbowe aondoke katika wadhifa alionao ili aweze kubaki na
nafasi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kinaonekana ni usaliti,”
alisema.
Aliongeza kuwa, siku za nyuma akiwa katika Jimbo la Karatu,
mkoani Arusha, Bw. Mbowe alimpigia debe Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt.
Wilbrod Slaa akidai atakuwa mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015 lakini
hakuonekana msaliti wa kauli iliyozusha sintofahamu miongoni mwa wanachama.
Akizungumzia sakata
la kuenguliwa kwenye nafasi yake kwa madai ya kutoa siri mbalimbali za chama,
alisema Kikao cha Baraza la Uongozi
Kanda ya Kaskazini hakina mamlaka ya kumuengua kwenye nafasi hiyo isipokuwa
Kamati Kuu ya chama hicho.
“Niliacha kazi yenye
mshahara wa sh. milioni 1.9, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) kutokana na mapenzi mema niliyonayo kwa CHADEMA.
“Nimewahi kukumbana
na misukosuko mingi pamoja na kukaa rumande siku saba kutokana na msimamo wangu
wa kuhamasisha mageuzi ya kweli,” alisema Bw. Mwigamba.
Hata hivyo, alisema
yeye ndiye kiongozi pekee ndani ya chama hicho aliyeandika makala nyingi kuliko
kiongozi yeyote kwa lengo la kuhamasisha mageuzi lakini hadi sasa anahukumiwa
kwa msimamo wa kutaka mabadiliko ya viongozi wanaoonesha kushindwa kukiongoza
chama hicho kimalengo.
Kikao cha baraza
hilo kilihudhuriwa na wabunge wote wa Kanda husika akiwemo Mwenyekiti wa
CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kilichofanyika Mjini Arusha.
Alisema tuhuma dhidi
yake ni kutumiwa na baadhi ya viongozi wa chama akiwemo Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe ili kukisambaratisha chama na kufafanua kuwa, madai hayo ni fikra
potofu za kisiasa.
“Tukiwa ndani ya
kikao, nilirushiwa tofali na Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, baada
ya hapo, red-briged (walinzi wa chama), walinikamata mbele ya Bw. Mbowe,
Mwenyekiti wa chama Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse, alisimama na
kusema kikao kinaahirishwa ili waweze kunijadili.
“Mbunge Lema hana
utu, anakosea sana kujiita mcha Mungu kwani amekuwa na tabia ya kuwachafua
baadhi ya viongozi wa chama nikiwemo mimi wakati elimu yake ni ndogo,” alisema.
Alisema alikijenga
chama hicho kwa kutumia rasilimali zake bila kuitendea haki familia yake na
kufafanua kuwa, Bw. Lema si mwanachama halisi katika chama.
Aliongeza kuwa, yeye
ni mwanachama hai na Mtanzania safi anayependa nchi yake na chama chake hivyo
kama viongozi wa chama wataamua kumruhusu amwage mchele kwa mambo yaliyotokea,
wamruhusu na hata shindwa.
CHADEMA wazungumza
Akizungumza na
Majira, Ofisa Habari wa CHADEMA, Bw. Tumaini Makene, alisema tukio lililotokea
Mjini Arusha na kusababisha Bw. Mwigamba kusimamishwa uongozi, halina uhusiano
wowote na Bw. Mbowe.
Alisema baraza hilo
la uongozi lilitoa uamuzi wa dharura kutokana na Bw. Mwigamba kuvunja kanuni,
maadili na taratibu za kikatiba za chama hicho kwani mamlaka hayo wanayo.
“Viongozi wa CHADEMA
ndiyo walioita polisi ili kumuokoa Mwigamba baada ya kukiri makosa aliyokuwa
akituhumiwa na alitia saini mwenyewe kwa dole gumba... katika kikao
kilichomsimamisha Mbowe hakuwepo.
“Huwezi kulifanya jiwe
liwe kichuguu hivyo kinachoelezwa juu ya jambo hili ni propaganda tu dhidi ya
Mwenyekiti wa chama kwani sisi tunaushahidi wa picha za mnato na video,”
alisema.
Aliongeza kuwa,
katika kikao hicho hakukuwa na vurugu ila baada ya Bw. Mwigamba kuambiwa atoke
nje na kushindwa kufanya hivyo, ndipo walipoitwa polisi kwa ajili ya usalama
wake mwenyewe.
Post a Comment