MBUNGE wa Viti Maalumu, Esther Bulaya
(CCM) amesema juhudi za Serikali kupambana na dawa za kulevya, zinazimwa
na baadhi ya watendaji wasio waaminifu katika Ofisi ya Mwendesha
Mashitaka (DPP), mahakimu na majaji.
Amesema
watendaji hao wasio na uzalendo, wanashirikiana na watuhumiwa wa dawa
za kulevya wenye kesi, kupanga jinsi ya kushinda kesi kwa kuwapa taarifa
za siri zinazohusu ushahidi na jinsi ya kuuharibu.
Bulaya
akitoa maelezo binafsi bungeni juzi, alisema mtandao uliopo katika
Ofisi ya DPP umekuwa ukituhumiwa kufanya njama za kushirikiana na baadhi
ya watumishi wa Mahakama, hasa majaji, kuhamisha kesi na kupeleka kwa
majaji wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo.
“Sina
haja kutaja majina ya majaji hapa, baadhi yao wanafahamika na wengine
wametajwa mara kadhaa na vyombo vya habari, lakini kwa kutumia mtandao
huo, baadhi yao wamekuwa wanatafsiri sheria jinsi wanavyotaka na kuwapa
dhamana watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya ambazo hazina dhamana,”
alieleza Bulaya.
Akitoa
mfano wa kesi hizo, Bulaya alitaja kesi namba 6/2011 ya Jamhuri dhidi
ya Fred William Chonde na wenzake, ambao walikutwa na kilo 179 za dawa
za kulevya aina ya heroine yenye thamani ya Sh bilioni 6.5
Alisema
washitakiwa hao, walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha dawa
za kulevya ambapo kwa mujibu wa sheria, hazina dhamana. Alitaja sheria
zinazozuia dhamana katika makosa hayo kuwa ni Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai, kifungu cha 148 (5), (a) (iii) na Sheria ya Kuzuia
Usafirishaji wa Dawa za Kulevya kifungu cha 27(1) (b).
Bulaya
alisema kwa tafsiri yoyote, Jaji hakupaswa kutoa dhamana kwa kuwa kosa
la kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani inayozidi Sh milioni 10,
halina dhamana.
Pamoja
na sheria hizo kutomwachia Jaji uhuru wa kutoa dhamana au la, Bulaya
alisema Mahakama ilitoa dhamana na washitakiwa hao raia wa Pakistani,
kwa sasa hawapo tena nchini, wametoroka. Kesi nyingine aliyoitaja ni ya
R.V. Mwinyi Rashid Ismail na Mkoko namba KLR/IR4143/2011, ambapo
mshitakiwa aliomba dhamana Mahakama Kuu, wakati kesi ilikuwa bado
Mahakama ya Kisutu.
Katika
kesi hiyo kwa mujibu wa Bulaya, jalada la kesi hiyo lilipofikishwa
Mahakama Kuu kwa ajili ya dhamana, wakati kesi ya msingi iko Kisutu,
Wakili wa Serikali alimwambia Jaji kuwa anataka kuifuta.
Waadhibiwe
Kutokana na udhaifu huo, Bulaya aliitaka Serikali kufanya mabadiliko ya
Sheria ya Dawa za Kulevya na kuanzisha Mahakama Maalumu ya
kushughulikia wahalifu wa dawa hizo.
Aliwasilisha
maelezo hayo chini ya kanuni ya 28 (8) ya Bunge toleo la mwaka 2013,
kuhusu tatizo sugu la uagizaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa hizo
linaloongezeka kwa kasi kubwa nchini kwa lengo la kuitaka Serikali
ichukue hatua hizo.
Bulaya
alisema ni wakati mwafaka kutoa maelezo hayo, ili Bunge na Serikali
wapate fursa ya kuona uzito wa tatizo la dawa za kulevya, kutokana na
ukweli, kwamba katika miaka ya karibuni tatizo hilo limeongezeka kwa
kasi ya ajabu hali inayosababisha athari kubwa za kiuchumi, kijamii na
kiafya nchini, huku kundi kubwa linaloathirika likiwa la vijana.
Utafiti
Bulaya alisema utafiti wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa (UN)
unaonesha kuwapo ongezeko kubwa na la kutisha, la matumizi ya dawa hizo
aina ya heroin kwa njia ya kujidunga katika Kenya, Libya, Mauritius,
Shelisheli na Tanzania.
Akinukuu
ripoti mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana
na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), alisema imetamka bayana, kwamba
Tanzania ina hali tete katika Afrika Mashariki na mkoa wa Tanga umo
hatarini zaidi.
Wabunge
waja juu Jana Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM)
aliomba Mwongozo wa Spika kuhusu maelezo binafsi ya Bulaya, juu ya
utendaji duni wa baadhi ya Mahakama na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama.
Alitaka
Serikali itoe jibu kuhusu hukumu za washitakiwa wa kesi za dawa za
kulevya na mustakabali wa Watanzania kwa usumbufu wanaopata kimataifa
hivi sasa.
Akijibu
hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, William Lukuvi,
alisema tayari Serikali inafanyia kazi suala hilo.
“Serikali
inajiandaa kutoa kauli yake bungeni kabla ya Bunge kwisha kupitia
Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu ufafanuzi wa namna inavyojipanga
kutekeleza hili, yaliyozungumzwa na Bulaya ndiyo tunayafanyia kazi sasa,
pia kuunda chombo kipya.Hata sisi tumejipanga na pia tutafafanua hoja
ya Bulaya,” alisisitiza Lukuvi.
Pamoja
na ufafanuzi huo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliomba
Mwongozo akihoji kwa nini Bunge lisitenge muda kujadili suala muhimu
kama hilo la dawa za kulevya kwa kutumia mamlaka ya kikanuni ya Spika.
Alisema
Bunge limekuwa likipoteza muda na kufanya mambo yasiyo muhimu ikiwemo
kuruhusu hata watu wasiohusika wala kuruhusiwa kuingia ndani ya Bunge
kama wachezaji wa mpira na wanafunzi waliofaulu vizuri, hivyo likubali
masuala kama hayo ya dawa za kulevya yajadiliwe.
Hata
hivyo, Naibu Spika Job Ndugai alimweleza Lugola kuwa, kanuni inaeleza
wazi, kuwa ni kwa idhini ya Spika ndipo maelezo binafsi yanaweza
kujadiliwa, na akafafanua kuwa Spika juzi aliona jambo hilo lisijadiliwe
na huo ndio uamuzi wa mwisho.
Post a Comment