Kwa ufupi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu na Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah
wamethibitisha.
Dodoma na Dar.Rais Jakaya Kikwete, kesho anatarajiwa
kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Habari zilizopatikana Mjini Dodoma jana na kuthibitishwa na
uongozi wa Bunge pamoja na Ikulu, Dar es Salaam zinasema atahutubia mchana.
Kutokana na ujio huo, Serikali imewaelekeza Mawaziri na
Manaibu Waziri kutotoka nje ya Dodoma hadi hapo Rais atakapokuwa amehutubia
Bunge. Kadhalika safari zote za Kamati za Bunge ambazo zilikuwa katika mchakato
wa kutekelezwa zimeahirishwa hadi baada ya kesho, ili kutoa fursa kwa wabunge
wote kuwapo wakati wa hotuba hiyo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kuwa
hata yeye amesikia taarifa kuwa Rais atazungumza bungeni lakini hajui
atazungumza kitu gani… “Hata mimi nimesikia kuwa atazungumza lakini sijui
atazungumza jambo gani kwa kuwa siyo miongoni mwa watu wanaomwandalia hotuba,”
alisema Balozi Sefue.
Kadhalika, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alithibitisha kuwa Rais Kikwete atalihutubia Bunge, Alhamisi… “Nathibitisha ni
kweli, ila kwa taarifa nyingine watafuteni watendaji wa Bunge, kama Katibu wa
Bunge nadhani wana taarifa zaidi.”
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alithibitisha jana
katika Viwanja vya Bunge Dodoma kuwapo kwa ratiba ya Rais Kikwete kulihutubia
Bunge na kwamba taarifa rasmi ingetolewa jana jioni kwa wabunge.
“Ni kweli Rais anatarajiwa kuja kulihutubia Bunge na leo
(jana) jioni, tutatoa taarifa rasmi bungeni,” alisema Dk Kashililah.
Mara ya mwisho Rais Kikwete alilihutubia Bunge wakati
akifungua rasmi Bunge la Kumi, Novemba 18, 2010 alipoeleza vipaumbele vya
Serikali yake katika awamu ya pili ya uongozi wake. Rais Kikwete analihutubia
Bunge wakati likisubiri kujadili mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa katika
mkutano uliopita.
Tayari Muswada wa Marekebisho unaopendekezwa umewasilishwa
katika Ofisi ya Katibu wa Bunge chini ya hati ya dharura na leo utajadiliwa
katika Kikao cha Kamati ya Uongozi ili kupata kibali cha kuingizwa ndani ya
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na baadaye Bungeni.
Dk Kashililah alisema amepokea muswada huo na kwamba uamuzi
wa lini utafikishwa bungeni utafanywa na Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo
itakutana na leo.
Kamati hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuifanyia marekebisho
ratiba ya vikao vya Bunge na kuruhusu mambo yanayopaswa kuingizwa bungeni
kujadiliwa.
Muswada huo ni matokeo ya majadiliano baina ya Serikali kwa
upande mmoja na vyama vya siasa vyenye wabunge chini ya uratibu wa Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) kwa upande mwingine, baada ya vyama vya siasa
kutoridhishwa na muswada ulipitishwa katika mkutano wa Bunge uliopita.
Itakumbukwa kwamba wabunge wa vyama vya upinzani vya
Chadema, NCCR Mageuzi na CUF walisusia shughuli za mchakato wa kupitishwa kwa
marekebisho ya sheria hiyo bungeni, hivyo kutoa fursa kwa wabunge wa CCM
kufanya watakavyo kisha kupitisha sheria hiyo.
Baada ya kupitishwa huko, vyama hivyo viliendesha kampeni ya
kuitisha maandamano nchi nzima, lakini kabla hayajafanyika Rais Kikwete
aliwaalika viongozi wake katika meza ya majadiliano, mchakato ambao umezaa
mabadiliko yanayokusudiwa kuingizwa bungeni wiki hii.
Katika mazingira hayo kumekuwa na hofu kwamba huenda wabunge
hasa wa CCM wakatumia wingi wao kukwamisha mabadiliko yanayopendekezwa kutokana
na kukasirishwa kwao na kile kilichoonekana kuwa ni Rais Kikwete kuwasikiliza
wapinzani.
Hiyo inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya Rais Kikwete kuamua
kulihutubia Bunge kwa lengo la kujenga msingi wa maridhiano katika mchakato wa
kuandikwa kwa Katiba Mpya kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
Post a Comment