NAIBU KATIBU MKUU WA CHADEMA, ZITTO KABWE, AMBAYE NI
MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)
Na Fredy Azzah, Mwananchi
Kwa ufupi
Vita hiyo ya maneno iliyoanzishwa na Lema katika kikao cha
wabunge wiki iliyopita kwamba Zitto anafanya unafiki kukataa posho, jana
iliingia katika hatua nyingine baada ya mwakilishi huyo wa Arusha kumshushia
tuhuma Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni,
lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Dar es Salaam. Vita vya maneno kati ya Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe imefika
pabaya.
Vita hiyo ya maneno iliyoanzishwa na Lema katika kikao cha
wabunge wiki iliyopita kwamba Zitto anafanya unafiki kukataa posho, jana
iliingia katika hatua nyingine baada ya mwakilishi huyo wa Arusha kumshushia
tuhuma Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni,
lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku
akisema kuwa, suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo
vya habari na hususani mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao
hiyo.
Katika hoja yake, Lema alisema kuwa Zitto ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) anakataa
posho ya Sh70,000 kwa kikao kimoja cha Bunge, lakini anapokea Sh700,000 mpaka
Sh1,000,000 kwa kikao kimoja cha kamati yake na haswa vile vinavyoandaliwa na
mifuko ya jamii.
Hata hivyo, zitto alikanusha shutuma hizo akimtaka Lema
kutoa ushahidi kama kuna mjumbe yoyote wa kamati ya PAC anayepokea posho, huku
akieleza kuwa hawezi kubishana na Mbunge huyo wa Arusha mjini kwani yeye Zitto
ni kiongozi wake ndani ya Chadema.
“Naomba kutaja masilahi yangu katika hili, wabunge wa
kawaida wakialikwa katika vikao hivyo huwa wanalipwa Sh500,000 kwa kikao kwa
siku . Mimi nimewahi kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo
pamoja na chai na chakula cha mchana.” alisema Lema.
Lema alisema posho hizo za wabunge ni tofauti na zile za
Mwenyekiti wa PAC kwani yeye pamoja na posho ya Sh700,000 mpaka Sh1,000,000
hupewa mafuta ya gari au tiketi ya ndege ya kumtoa alipo na kumrudisha na
kukodiwa hoteli yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa siku gharama
yake ni Dola za Marekani 100 mpaka 600 kwa siku .
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwisha
piga marufuku kwa PAC kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa
na kamati hiyo.
“Toka nimekuwa Mwenyekiti wa POAC (Kamati ya Hesabu za
Mashirika ya Umma) sio tu nilipiga marufuku posho bali pia niliwashitaki PCCB
(Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa) wabunge wanaochukua posho kutoka kwa
taasisi za Serikali,” alisema Zitto.
Alieleza baada ya hatua hiyo, wabunge walihojiwa na PCCB
kuhusu jambo hilo mpaka aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Samuel Sitta
alipoingilia kati na kuwatetea wabunge hao.
“Hiyo ilikuwa mwaka 2009 kabla hata Lema hajawa mbunge,
wajumbe wa kamati ya PAC wanalipwa posho za vikao kama wabunge wengine, lakini
mimi sichukui posho hizo za vikao,” alisema na kuongeza:.
“Sio tu PAC hata kwenye Baraza la Madiwani na Baraza la
Mashauriano la Mkoa wa Kigoma na popote kule. Hata NGO (Mashirika yasiyo ya
Kiserikali) zikinialika kwenye vikao vyao sichukui posho za vikao. Nafasi
yoyote ninayoalikwa kama mbunge sichukui posho za vikao,” alisema Zitto.
Alisema mtu yeyote mwenye ushahidi wa yeye kuchukua posho za
vikao popote pale auweke hadharani na atawajibika.
“Sio kuandika uzushi au maneno ambayo mtu yeyote anaweza
kuandika. Mimi siwezi kubishana na Lema maana ni kiongozi wake katika chama.
Natumaini kadiri anavyokaa kwenye uwanja huu wa siasa atabadilika na kukomaa
zaidi,” alisema Zitto.
Kwenye hoja yake, Lema alisema kuwa Chadema walikuwa
wanakataa posho na kupendekeza mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima
ziondolewe ili kuondoa mwanya wa ubadhirifu wa fedha za umma.
“Huu ndio uliokuwa msimamo wetu kulikuwa na msingi mkuu
ambao ungekuwa na faida kubwa kwa nchi na watu wake,” alisema Lema.
Lema alisema kwamba kabla msimamo huu haujawekwa hadharani
na kutafsiriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto tayari alishatoka
katika vyombo vya habari na kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala
hatachukua posho.
Lema alisema kuwa, anaamini kuwa umaskini siyo uzalendo.
“Sipendi umaskini, nachukia umaskini, pia sipendi kuona mafanikio yangu
yanabaki kwangu tu huku wengine wakiteseka, lakini siwezi pia kukumbatia
umaskini kwa lengo lakuthibitisha uzalendo wangu.
Najua watu wa jimbo langu wanataka maji , umeme na huduma
bora za afya na mambo mengi yenye sura hii, lakini sitang’oa bomba la maji
nyumbani kwangu kwa sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa kadiri
nitakavyoweza na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji,” alisema Lema .
Post a Comment