Spika wa Bunge Anna Makinda akiongoza shughuli za Bunge
Bungeni, mapema wiki iliyopita baadhi ya wabunge walikuja na hoja ya kutaka
kumng'oa Spika huyo bungeni. Picha na Maktaba
Na Neville Meena, Mwananchi
Kwa ufupi
Licha ya kukwama
kupata saini za baadhi ya wabunge, Dk Kigwangalla ametamba kupata saini za
wabunge 110 katika kutimiza azma yake ya kumng’oa Spika Makinda
Dodoma. Mchakato wa kumng’oa madarakani Spika wa Bunge, Anne
Makinda ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla (CCM),
huenda usifanikiwe kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo kupingwa na baadhi ya
wabunge wenye ushawishi mkubwa katika Bunge.
Wabunge wameanza kumpinga hadharani kuhusu suala hilo ambalo
jana mjadala wake uliyateka makundi ya wabunge waliokuwa wakihudhuria vikao vya
kamati mbalimbali wakati wakiwa kwenye mapumziko.
Katika viwanja vya Bunge jana, gazeti hili liliwashuhudia
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na swahiba wake kisiasa, Kangi Lugola
ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) wakikataa kusaini karatasi waliyopelekewa
kuunga mkono kung’olewa kwa Spika.
Baadaye kwa nyakati tofauti walisema “hoja hiyo haina
mashiko” na kwamba hawakutumwa na wapigakura wao kuwania posho bungeni.
Wabunge hao walikuwa wakirejea moja ya hoja za Dk
Kigwangalla kwamba Makinda amekiuka kanuni kwa kuidhinisha malipo ya Sh430,000
kama posho kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na wajumbe wa
kamati nyingine ambao malipo yao ni Sh180,000 kwa siku.
Wengine wanaompinga Kigwangalla ni Mbunge wa Tabora Mjini,
Ismail Aden Rage (CCM) na yule wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR -
Mageuzi), ambao pia walisema hawaoni sababu za msingi za kumwondoa Makinda
madarakani.
Rage kwa upande wake alisema haoni sababu za msingi za
kutaka kumwondoa madarakani Makinda, wakati Kafulila alisema hilo ni suala la
WanaCCM, kwani hata Spika aking’olewa atakayeziba pengo hilo hawezi kutoka
upinzani.
“Kama akitoka Makinda ataingia mtu wa opposition (upinzani)
yeyote basi ningeweza kusaini, lakini ninachojua ni kuwa kama wakifanikiwa
kumtoa watakaa kwenye Party Caucus (kikao cha chama) na watateua mwingine
kutoka miongoni mwao na mimi simwamini mbunge yeyote wa CCM,” alisema Kafulila.
Filikunjombe na Lugola
Kwa upande wake Filikunjombe alisema hoja ya Dk Kigwangalla
imejengwa katika msingi hafifu na kwamba “haizingatii masilahi mapana ya nchi,
bali masilahi binafsi kwa mtazamo finyu wenye lengo la kujitafutia umaarufu”.
“Bunge ni taasisi kubwa ambayo haiwezi tu kuingia katika
mtego wa kuenguana kwa sababu ya posho. Watu wa Ludewa watanishangaa leo hii
wakisikia kwamba eti nimesaini kumwondoa Spika madarakani kwa sababu ya posho,”
alisema Filikunjombe na kuongeza: “Kama hoja ingekuwa ni kumtoa Spika kwa
sababu anaipendelea na kuitetea Serikali bungeni kana kwamba yeye ni waziri,
basi hoja kama hiyo mimi ningeweza kuiunga mkono, lakini siyo suala la posho”.
Kuhusu hoja kwamba Spika Makinda alikiuka kanuni kwa kumteua
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti
badala ya kuchaguliwa kwa kura, Filikunjombe alisema wanaopaswa kulalamika
kwanza ni wajumbe wa kamati hiyo na siyo mtu mwingine yeyote.
Kwa upande wake Lugola alisema msingi wa hoja ya Dk
Kigwangalla ni masilahi binafsi na kwamba ni mapambano ya kuwania kupata
kiwango kikubwa cha posho, suala ambalo kwa sasa siyo ajenda ya kitaifa.
“Kama kweli mtoa hoja angekuwa ana nia ya dhati na uchungu
wa nchi hii, angetuunga mkono katika hoja ya kutaka kumwondoa Waziri Mkuu,
lakini hakufanya hivyo sasa iweje leo anataka tumuunge mkono katika masuala ya
posho?” alihoji Lugola.
Wabunge hao walisema fedha wanazipenda, lakini siyo
kipaumbele katika kutekeleza yale waliyotumwa na wanaowawakilisha bungeni. Hata
hivyo Dk Kigwangalla aliwapuuza wabunge hao akisema kuwa anayetaka asaini na
asiyetaka asisaini na siyo kumshambulia na kumbeza.
Vikwazo vingine
Mchakato wa kutaka kumg’oa Spika pia unaweza hata usifike
katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na badala yake kuishia
Ofisi ya Katibu wa Bunge ambako bado hoja yake inafanyiwa kazi na wataalamu wa
ofisi hiyo.
Hadi jana mchana Dk Kigwangalla alikuwa bado hajapokea
majibu kutoka ofisi ya katibu huyo na aliliambia gazeti hili kuwa Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashililah alimwarifu kuwa “wataalamu walikuwa bado
wanaifanyia uchambuzi hoja yake hiyo”.
Dk Kashililah kwa upande wake aliliambia Mwananchi Jumapili
kuwa: “Ni kweli hoja yake (Dk Kigwangalla) tumeipokea na tunaifanyia kazi,
tukimaliza tutamwarifu matokeo ya uchambuzi wetu”.
Wakati Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akisubiri majibu kutoka Ofisi ya
Katibu wa Bunge, alisema tayari alikuwa amekusanya saini za wabunge wapatao 110
ambao wanamuunga mkono katika harakati zake.
Miongoni mwa hoja za mbunge huyo ni kwamba Spika amekuwa
akivunja masharti ya Kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na
kujadili jambo la dharura kwa kuzuia mijadala hiyo.
Hata hivyo hatua ya Spika Makinda kuruhusu mijadala kuhusu
migogoro baina ya wakulima na wafugaji na ile inayohusu utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili juzi, inaweza kutumika kama kigezo cha kuiweka
kando hoja ya Dk. Kigwangalla.
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema katika
mazingira hayo, Ofisi ya Katibu wa Bunge inaweza kutumia sababu hiyo pamoja na
nyingine za kiufundi kuiweka kando hoja mbunge huyo, na kuzuia isipelekwe
katika kamati husika kama kanuni zinavyoelekeza.
Kikwazo kingine ni ukimya wa Kambi ya Upinzani Bungeni
ambayo hadi sasa imekaa kimya, ikiwa ni dalili ya kuwaacha CCM “waumane” wao
kwa wao.

Post a Comment