
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyeshika mkasi) akikata
utepe kuzindua rasmi ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo. Kushoto kwa
Rais ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John P. Magufuli na kulia kwa Rais ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Alhaj Eng. Mussa Iyombe. Wengine katika picha ni
baadhi ya Mawaziri, Wabunge na Viongozi wa Mikoa ya Geita na Kagera
walioshiriki katika sherehe hizo.

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na Waziri wa
Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa
barabara ya Bwanga – Biharamulo.

Lori aina ya Scania la Kampuni ya MAP CO Ltd. likiwa na
usajili namba T 895 AFH/T 226 AGB kama
lilivyokutwa eneo la Manyoni mkoani Singida likiwa limekatika katikati
kutokana na kuelemewa na uzito wa mzigo lililoubeba.
-----------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete amemtaka Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli
kuhakikisha kuwa Sheria ya Usalama Barabarani inasimamiwa vizuri ili
kuhakikisha kuwa barabara zinazojengwa nchini zinadumu kwa muda uliokusudiwa.
Akizungumza katika eneo la Buziku mkoani Geita wakati
akizindua ujenzi wa barabara ya Bwanga hadi Biharamulo yenye urefu wa kilometa
67, Rais Kikwete alisema kuwa wizara ya Ujenzi ni lazima ihakikishe inasimamia
sheria zilizopo na hasa hii ya kutoruhusu magari yenye uzito uliozidi viwango
vilivyoainishwa katika Sheria Namba 30 ya Mwaka 1973.
Akisistiza umuhimu wa kutunza barabara Rais Kikwete
alibainisha kuwa “adui wakuu watatu wanao sababisha barabara kuharibika mapema
ni; magari yanayobeba mizigo zaidi ya uzito uliowekwa kisheria, ujenzi duni
usiozingatia viwango na kuachwa kwa maji kuzagaa barabarani”.
Wakati huo huo Rais Kikwete alielezea kufurahishwa kwa
kuanza ujenzi wa mradi huo kwani wapo baadhi ya watu waliokuwa waliokuwa wakieneza
taarifa kuwa sehemu hiyo ya barabara haiwezi kujengwa lakini sasa wameumbuka.
Awali akitoa maelezo ya mradi huo Mtendaji Mkuu wa Tanroads
Injinia Patrick Mfugale alielezea kuwa mradi mradi wa ujenzi wa barabara hiyo
kwa kiwango cha lami umegharimu Shilingi bilioni 55 fedha zote zikiwa
zimetolewa na Serikali ya Tanzania. “Mradi huu utajengwa kwa muda wa miezi 27
na hivyo kukamilika mwezi Februari mwaka 2015” alisema Injinia Mfugale.
Naye Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Magufuli alimhakikishia Rais
Kikwete kuwa wizara yake itahakikisha kuwa inamsimamia mjenzi wa mradi huo
ambaye ni Kampuni ya Sinohydro Ltd. ya kutoka Jamhuri ya Watu wa China ili
aukamilishe kwa muda na viwango vilivyokusudiwa na bila ya visingizio vya
nyongeza ya gharama.
Akimpongeza Rais kwa kutekeleza ahadi yake, Waziri Magufuli
alibainisha kuwa wananchi wa mikoa ya
Geita na Kagera wamefurahishwa sana kuona kuwa hatimaye barabara hiyo muhimu
inajengwa kwani hiyo ndiyo sehemu pekee iliyokuwa imebaki ikiwa haina lami kwa
barabara inayounganisha mikoa hiyo ya ziwa.

Post a Comment