Miss Universe Tanzania, Betty Boniface akionyesha vazi lake la ubunifu wakati wa mashindano ya Miss Universe World yaliyofanyika Russia hivi karibuni. Picha na AFP.
Na Imani Makongoro, Mwananchi
Kwa ufupi
Miss Universe, Betty alikuwa Russia kwenye mashindano ya Miss Universe dunia yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu na Maria Gabriela Isler wa Venezuela kunyakuwa taji la Miss Universe 2013.
Miss Universe Tanzania, Betty Boniface amesema pamoja na kutofanikiwa kuingia hatua ya 16 bora Miss Universe Dunia, anajivunia kutangaza utalii wa Tanzania.
Miss Universe, Betty alikuwa Russia kwenye mashindano ya Miss Universe dunia yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu na Maria Gabriela Isler wa Venezuela kunyakuwa taji la Miss Universe 2013.
Betty aliyeng’ara katika vazi la Taifa kwa kuvaa vazi la mkeka lililobuniwa na mbunifu chipukizi, Mwanakombo Salim kwa kusaidiana na wasanii wa Tingatinga, alisema kuwa pamoja na kutofanikiwa kuingia hatua ya 16 bora, anachojivunia ni kuitangaza nchi kwa kupitia vivutio vya utalii akiwa balozi wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) ambao walikuwa wadhamini wakuu wa mashindano ya Miss Universe Tanzania.
Alisema katika mashindano hayo alikuwa mrembo pekee kutoka bara la Afrika aliyechaguliwa miongoni mwa warembo nane kote ulimwenguni kushiriki katika kipindi maarufu mjini Moscow kinachoonyeshwa duniani kote kijulikanacho kama “Let Them Talk” kinachoendeshwa na mtangazaji maarufu Andrey Malakhov.
Betty alisema kuwa katika kipindi hicho ambacho kinapatikana kwenye mtandao, alionekana kuwafurahisha sana hadhara ya warusi katika studio na kusifiwa kwa kuwa mrembo wa kipekee na mwonekano wake wa kiafrika.
Alifafanua kuwa baadhi ya majaji wa mashindano ya Miss Universe walikuwepo na walieleza kuvutiwa na Betty na kumwona kama mrembo ambaye alikuwa ana nafasi kubwa ya kuingia 16 bora.
“Kipindi chote nilipokuwa Russia, niliona kukubalika na Warussia wenyewe na hata vyombo vya habari vya kimataifa. Nina furaha kubwa sana kwani kilichonileta nimekifanikisha kwani lengo langu kubwa zaidi ya ushindi ilikuwa ni kuhakikisha naitangaza vyema Tanzania na vivutio vyake, kama vile hifadhi za taifa za Ruaha, Udzungwa, Katavi na mengineyo” alisema Betty.
Alisema kuwa kwa msaada mkubwa wa ubalozi wa Tanzania nchini Russia, alifanikiwa kufanya mahojiano na gazeti maarufu la utalii nchini humo lijulikanalo “Hot Line travel Magazine.
Post a Comment