Baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa Zitto Kabwe, mama yake mzazi Shida Salum (pichani) aibuka kueleza jinsi zahama hiyo ilivyokuwa ‘ushindi’ kwa mwanae. PICHA | MAKTABA
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Kwa ufupi
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu, Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu kila siku ili afukuzwe Chadema,” alisema Mama Zitto wakati akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Tabata, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu, Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu kila siku ili afukuzwe Chadema,” alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye na kusisitiza, “Watu walikaa na kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto na kuiweka kwenye mtandao kisha kuituma kwa wanachama wa Chadema wanaowafahamu. Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini wameshindwa.”
Alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa amemnyang’anya mwanaye kwa muda simu zake zote za mkononi, kompyuta mpakato (Laptop) pamoja na iPad ili asiwasiliane na watu, kwa maelezo kuwa wapo wenye nia mbaya wanaomsaka kumpa pole za kinafiki. “Kwa sasa nataka mwanangu atulize akili.”
Shida Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, pia ni mwasisi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (Chawata).
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo juzi walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20 mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kukisaliti chama.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Katika ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka wanachama wa Chadema kuwa watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa uanachama, “Siku nyingi walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo Chadema wanasema amefanya, hawana uhakika nalo.”
Juzi wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
Alisema kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne ambaye alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina la M2.
Atoa ya moyoni
Mama Zitto ambaye wakati akizungumza na gazeti hili alikuwa amelala kutokana na kusumbuliwa na maradhi alisema, “Kutolewa katika uongozi ni jambo la kawaida. Zitto hajafukuzwa chama ila anaweza akafukuzwa maana kapewa siku 14 tu za kujieleza.”
Alisema kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, kwamba chama hicho walimwondoa Aman Kabourou (aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini-Chadema) itakuwa Zitto, inaonyesha jinsi watu walivyo na chuki na mwanaye.
“Hayo ni maneno ya chuki, maana hata Zitto naye ana watu wake ambao wanaweza kutengeneza aina fulani ya chuki kwa viongozi wa chama na wanaweza kupata wakati mgumu kufanya safari au mikutano yao mikoani,” alisema.
Alisema tangu siku nyingi ndani ya Chadema kulikuwa na mpango wa kumng’oa Zitto, akifafanua kuwa hata katika kikao cha Kamati Kuu iliibuliwa hoja ya ruzuku za vyama, huku wajumbe wakimshutumu Zitto kwamba kwa nafasi yake na Naibu Katibu Mkuu alitakiwa kuitetea Chadema kuhusu ruzuku.
Katika vikao vya Kamati ya PAC, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
“Zitto alipoingia katika kikao cha Kamati Kuu alishikilia msimamo wake kwamba kama Chadema inachukia ufisadi, nacho lazima kihakikishe kinakaguliwa,” alisema na kuongeza;
“Wao wanaona ili waweze kusalimika katika suala hili la ruzuku ni lazima wamfukuze Zitto. Chadema hawako sawa, hesabu zao haziko sawa.”
Alisema kuwa tatizo lililopo ni kuwapo kwa mkakati wa watu fulani kuiyumbisha Chadema , hivyo kila juhudi zinafanywa ili kukitingisha chama hicho kipoteze mwelekeo.
“Siwezi kusema wamemwonea au hawajamwonea, wao wametumia waraka wa Mwigamba ambao Zitto amekiri katika Kamati Kuu kwamba hajawahi kuusikia wala kuuona, tofauti na Dk Kitila ambaye amesema amewahi kuuona,” alisema na kuongeza;
“Zitto anahusishwa na kitu ambacho Chadema hawana uhakika nacho, ukiusoma ule waraka katika aya ya mwisho umeandikwa hivi, ‘Huyu mtu tunayefikiria awe mwenyekiti hajaoa,
tumshauri aoe akikataa tutafute mtu mwingine’, maana yake ni kwamba waraka huo ulikuwa haujamfikia Zitto, kama ungekuwa umemfikia Zitto watu hao wasingemwomba Zitto agombee uenyekiti.” Alipoulizwa nafasi yake ndani ya Chadema kutokana na yaliyomkuta mwanaye alisema, “Mimi hawawezi kunitengenezea jambo. Hivi Zitto anaweza kuwa mbaya mimi nikawa mzuri.”
Mama huyo alieleza kuwa tangu alipovamiwa na majambazi nyumbani kwake, Aprili 19 mwaka huu hajawahi kuhudhuria kikao chochote cha Chadema. “Wale wanaodhani Zitto kaonewa wanatakiwa kuwa wavumilivu na wapole, wasubiri kwani kila kitu kinawezekana.”
Ushauri kwa mwanaye
Alisema kuwa mwanaye ana uamuzi wake na kwamba hata kama Chadema itamfukuza uanachama, haitaweza kumnyang’anya vyeti vyake vya elimu aliyoipata.
“Zitto anaweza kufanya kazi mahali popote duniani, lakini pia ni mwalimu anaweza kuamua kufundisha. Ubunge ni mgawanyo wa madaraka. Watu wote hatuwezi kuwa wabunge,” alisisitiza.
Alisema wakati Kikao cha Kamati Kuu kikifanyika Zitto alikuwa nje ya nchi na kwamba yeye alimshauri kuhakikisha kuwa anahudhuria kikao hicho.
“Alipotua tu na ndege aliniambia kuwa kuna foleni na alitaka kukodi pikipiki ili awahi kikao, aliniambia lazima aende ili kujua hatima yake.
Aliacha gari lake na kwenda na hata mimi nilimsisitizia kwamba ni lazima aende katika kikao,” alisema. Alisema kuwa Zitto alipofika katika kikao hicho aliweza kuzima hoja zote zilizomhusu ikiwamo ya ruzuku za vyama, kwamba baadhi ya wajumbe walipoona amebadili mwelekeo wa kikao, mjumbe mmoja (akamtaja kwa jina) aliibua waraka uliomng’oa Zitto katika wadhifa wake.
“Unajua Kamati Kuu ilijadili zaidi kuhusu ruzuku. Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora Mwigamba laptop yake alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha Chadema,” alisema.
Huku akiwataja wanachama wa Chadema walioongeza maneno katika waraka huo (wakiwamo wabunge wawili) na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, mama Zitto alisema kilichomkuta mwanaye ni ushindi mkubwa, kwamba alipangiwa kufanyiwa makubwa zaidi ya yaliyomkuta.
“Hakuna amani maana ukisikia kengele inagongwa hapa nyumbani unasema hao ndiyo wamekuja kumuua Zitto nini, hivi sasa mpaka walinzi wanaolinda hapa wakisikia unakuja nyumbani kwa Zitto lazima wakuandike jina na kukufuatilia,” alisema mama huyo.
Dk Kitila alonga
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mkumbo alisema kutokana na ushauri wa watu mbalimbali, yeye na Zitto wamepanga kukutana na waandishi wa habari na kutoa tamko.
“Tumepanga mimi na Zitto tutatoa ufafanuzi kuhusu jambo hili, nadhani ni kesho (leo), tutawajulisha lakini,” alisema.
Baada ya chama hicho kutangaza kuwaengua katika uongozi Zitto na Dk Kitila, saa mbili baadaye Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Said Arfi aliandika barua ya kujiuzulu.
Post a Comment