ZANZIBAR NOVEMBA 15, 2013. Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata watuhumiwa wemgine watatu wakiwemo Maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato nchini TRA kituo cha Bandari Zanzibar kwa kuhusika na kashfa ya kupatikana kwa meno ya tembo yenye thamani ya Mabilioni ya shilingi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amewataja Maafisa hao wa TRA waliokamatwa kuwa ni Omari Hamad Ali(50) na Mohammed Hija(48) ambao wote wanafanyia kazi katika Bandari ya Zanzibar. Mtuhumiwa mwingine ni kibarua wa Mamlaka ya bandari Zanzibar Haidar Ahmad Abdallah(54).
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa kwa kuhusika na sakata hilo kufikia watano.
Tayari watuhumiwa hao wamesafirishwa kwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi.Pamoja na mambo mengine, kusafirishwa kwa watuhumiwa hao kwenda Jijini Dar es Salaam, kunatokana na Zanzibar kutokuwa na Sheria maalumu inayohusu wanyamapori.
Maafisa wa Idara ya Wanyamapori nchini, leo wamekamilisha kazi ya kuhesabu na kulinganisha vipande 1,023 vya meno ya tembo vilivyokamatwa jana kwenye Bandari ya Zanzibar na kubaini idadi ya tembo waliouawa kuwa ni 305.
Hadi sasa bado Makachero wa Polisi wa Kimataifa Interpol hapa nchini kwa kushirikiana na Makachero wa Polisi Zanzibar, idara ya wanyamapori makao makuu wanaendelea na upelelezi wa kuwabaini wale wote waliohusika na kashfa hiyo.
Jana Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kuwa upelelezi wa kina unafanyika ili kuwakamata wale wote wanaohusika na mtandao huo.
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi bado linamsaka tajiri aliyewezesha mipango ya kukusanywa na kusafirisha shehena hiyo kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar ili kusafirishwa nje ya nchi.
Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Post a Comment