Home » » Uchaguzi mdogo janga Chadema

Uchaguzi mdogo janga Chadema

Written By JAK on Tuesday, February 11, 2014 | 10:08 AM

 
Dk Kitila Mkumbo
 
MATOKEO ya uchaguzi mdogo uliofanyika nchi nzima katika kata 27, zilizopo ndani ya mikoa 15 na kuipa CCM ushindi yamerejesha kilio katika uongozi wa Chadema.

Uchaguzi huo umefanyika wiki moja baada ya kumaliza Operesheni ya M4C Pamoja Daima, iliyofanyika kwa helikopta tatu zilizozunguka nchi nzima.

Mbali na kurusha helikopta tatu kwa mara ya kwanza katika historia ya chama hicho, uchaguzi huo pia umefanyika siku chache baada ya kuibuka kwa mpasuko ndani ya chama hicho.

Katika jitihada za kuziba mpasuko huo viongozi wa kitaifa wanaounga mkono uongozi wa Mwenyekiti, Freeman Mbowe, akiwamo yeye mwenyewe, Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa, Msemaji wa Chama, John Mnyika na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu, walizunguka nchini kujaribu kuponya mpasuko huo bila mafanikio.

Pamoja na ziara hizo na Operesheni ya M4C Pamoja Daima kujaribu kuelewesha Watanzania kuwa Chadema ni chama mbadala, kinachojiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na kuchukua Dola katika Uchaguzi Mkuu mwakani, matokeo ya uchaguzi wa juzi yalitoa picha tofauti ya nguvu zinazodhaniwa kuwa ni za Chadema nchini.

Katika uchaguzi huo chama hicho kiliweka wagombea katika kata zote 27, kwenye mikoa 15, lakini kilijikuta kikiambulia ushindi katika kata tatu tu za mikoa miwili ya Arusha na Kilimanjaro ambako ni ngome kuu ya chama chicho na moja katika Mkoa wa Njombe.

Mafanikio pekee yaliyoonekana, ambayo yamepewa jina la ‘Chopa tatu, kata tatu’ ni ushindi wa Chadema katika kata ya Sombetini, Arusha na Njombe Mjini mkoani Njombe, ambazo zilikuwa zikiongozwa na CCM.

Kata ya Kiboroloni mkoani Kilimanjaro, ilikuwa ya Chadema na imeitetea. Hata hivyo, Chadema imepoteza kata mbili za Nyasura mkoani Mara na Mkongolo, Kigoma ambazo zimechukuliwa na CCM.

Madai ya akina Kitila Ufanisi hafifu wa Operesheni ya M4C Pamoja Daima uliodhihirishwa na matokeo ya uchaguzi mdogo, umethibitisha matokeo ya utafiti wa aliyekuwa Mshauri Mkuu wa Chama hicho, Dk Kitila Mkumbo, ambaye ndiye pia aliyeandika Ilani ya Uchaguzi ya Chadema.

Dk Mkumbo katika utafiti wake aliouita wa kisayansi, alibaini kuwa uongozi uliopo umechoka na uchovu huo umekuwa ukionekana dhahiri katika mipango na mikakati ya Chadema ya miaka kadhaa.

“Mfano mwaka 2008 uongozi ulianzisha mkakati wa Operesheni Sangara. Huo ulifanyiwa kazi katika mikoa kadhaa na hatimaye kufa kimyakimya. “Baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 kulianzishwa matembezi ya maandamano ambayo nayo yalikuwa yakipeleka ujumbe kwa watu na yalipangwa kufanyika mikoa yote na wilaya zote.

“Kumbukumbu zetu zinaonesha, kwamba maandamano hayo yalipaswa kuanzia makao makuu ya mkoa na kufika wilaya zote. Lakini kumbukumbu hizo zinaonesha kwamba yalifanyika Mwanza, Musoma, Shinyanga, Kagera na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa), kisha yakafa ‘kifo cha mende’.

Dk Mkumbo katika utafiti huo, alibainisha kuwa mwaka 2012 ilianzishwa operesheni ya mabadiliko maarufu ya Movement for Change (M4C).

Hiyo ilikuwa inakwenda mikoani na timu kama nne ambazo kwa ujumla zilitathmini hali ya mtandao na uongozi wa chama, kuhamasisha umma kwa njia ya mikutano ya hadhara, kuingiza wanachama na kusimika uongozi na hatimaye kufanya mafunzo kwa viongozi. Alieleza kuwa hiyo ilifanyika Mtwara na Lindi, Morogoro na kufia Iringa.

“Mafanikio yetu kwenye uchaguzi mdogo nayo ni ishara, kwamba mabadiliko yanahitajika. Tangu uongozi huu uingie madarakani, kumefanyika uchaguzi mdogo mara nane wa wabunge, tumeshinda mbili tu sawa na asilimia 25. “Aidha, baada ya mwaka 2010 kulifanyika uchaguzi kadhaa wa wawakilishi kwenye halmashauri (madiwani).

Oktoba 2011, Aprili 2012, Septemba 2012 na Juni 2013. Kote mafanikio yetu yamekuwa hafifu kupindukia. “Mfano Juni 2013 tulipata viti sita kati ya 22 (27%) na Septemba 2012 viti saba kati ya 29 (24%),” alisema Dk Mkumbo.

Uchaguzi wa juzi Chadema ilipata viti vitatu kati ya 27. “Tunahitaji mbinu mpya. Kwa kifupi, ushindi ambao tumekuwa tukiupata katika uchaguzi mdogo haulingani na ukubwa wa hamasa wa Chadema uliopo mitaani.

 Hii ni kwa sababu tumekuwa tukitumia mbinu hizohizo katika kila uchaguzi,” alisema Dk Mkumbo.

Majimbo hatarini

Hatua ya Chadema kutumia kukubalika kwa wabunge wake wa majimbo katika mikoa hiyo 15 iliyokuwa ikifanya uchaguzi mdogo wa udiwani na kuishia kupata kata tatu, huku ikipoteza mbili, imeanza kuhusishwa na uwezekano wa kupoteza baadhi ya majimbo katika uchaguzi mkuu ujao. Jimbo la kwanza lililo rehani Chadema, ni Iringa Mjini, ambalo kwa sasa linaongozwa na Peter Msigwa.

Katika mkoa huo uchaguzi ulifanyika katika kata ya Nduli, Iringa Mjini na kata za Ukumbi na Ibumu wilayani Kilolo na kote CCM imeshinda.

Mbali na Msigwa kutumia nguvu ushawishi katika uchaguzi huo, Dk Slaa na viongozi wengine walitua na helikopta kuongeza nguvu, lakini vyote havikufua dafu.

Tayari

Katibu wa CCM wa Manispaa ya Iringa, Hassan Mtenga ametoa tamko, kwamba ushindi huo unatoa mwelekeo mzuri kwa chama chao kurejesha Iringa Mjini, ujumbe ambao si mzuri kwa Msigwa.

Ujumbe wa CCM kwa Chadema kwa mujibu wa Mtenga, utakwenda sambamba na mikutano mikubwa ya kushukuru wananchi kwa kuichagua CCM katika uchaguzi huo.

Jimbo lingine lililo hatarini ni Mbeya Mjini la Joseph Mbilinyi (Chadema).Jimbo hilo ndiko CCM iliamua kupatumia kuwa sehemu ya kilele cha sherehe za kutimiza miaka 37 ya kuzaliwa kwake.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwa makusudi, alitumia muda wa kuhutubia wanaCCM na Taifa, kufafanua mafanikio ya Ilani ya CCM Mbeya.

“Kwa hapa mkoani Mbeya, nawapongeza kwa kupiga hatua nzuri ya maendeleo katika maeneo mbalimbali. Kwa upande wa elimu mmefanikiwa kupanua fursa za elimu katika ngazi zote. Mkoa una shule za msingi 1,094 zenye wanafunzi 532,765, shule za sekondari ni 310 zenye wanafunzi 152,289; vyuo vikuu vitatu na matawi kadhaa ya vyuo vikuu na vyuo sita vya ualimu. Kazi mliyonayo ni kuwasimamia na kuwaongoza vijana wetu watumie ipasavyo fursa hizo.

“Kwa upande wa afya, upanuzi wa hospitali ya mkoa unaendelea vizuri na majengo ya hospitali na wadi yanaendelea kujengwa. Mwaka wa fedha 2013/14 zaidi ya Sh milioni 300 zimetengwa kumalizia ujenzi wa wadi ya watoto na mkandarasi wa kuifanya kazi hiyo tayari amepatikana. Suala la ghala la Bohari ya Dawa (MSD) ndani ya hospitali tutalipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo.

“Kuhusu maji, kwa mwaka 2013/14 miradi 80 ya maji inatekelezwa katika vijiji 112 ambapo kati ya hiyo miradi 15 imekamilika. Miradi hiyo ni Namkukwe (Chunya), Namtambalala (Momba), Masoko (Kyela), Kyimo (Rungwe), Mbambo, Kipapa na Kikuba (Busokelo), Ubaruku na Chimala (Mbarali), Mbebe na Luswisi (Ileje), Ikombe (Kyela), Maninga (Mbozi), Iwalanje na Shongo/Igale (Mbeya).

“Miradi mingine 55 iko katika hatua za ujenzi na mingine 10 katika hatua za zabuni. Jumla ya Sh bilioni 38.14 zinategemewa kutumika katika ujenzi wa miradi hiyo itakayohudumia watu wapatao 508,064. 

“Itakapokamilika itafanya huduma ya maji vijijini kufikia asilimia 73.5. Kwa hapa mjini nafahamu hali ya upatikanaji wa maji safi na salama inaridhisha. Ombi langu kwenu, tunzeni vyanzo vya maji ili upatikanaji maji uwe wa uhakika,” alisema Kikwete, akijua fika Chadema ndio wanaongoza Mbeya Mjini.

Kabla ya hotuba hiyo ya Mwenyekiti wa CCM, mmoja wa makada wa CCM Mbeya, Profesa Mark Mwandosya, alitamba kuwa Mbeya Mjini itarejeshwa CCM.

Matokeo ya juzi, pamoja na Mbunge Mbilinyi kufanya mikutano na helikopta ya M4C ikiwa na Mwenyekiti Mbowe kufanya ziara, kata za Malindo na Santilya, zilirejeshwa CCM.

Ufa Baraza Kuu

Matokeo hayo ya uchaguzi mdogo, ni pigo lingine kwa uongozi wa Mbowe na wafuasi wake ndani ya Chadema na unatafsiriwa kuwa ushindi kwa wafuasi wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.

Zitto ameweka zuio Mahakama Kuu dhidi ya Kamati Kuu ya Chadema yenye ushawishi mkubwa wa Mbowe, isijadili wala kuamua lolote kuhusu uanachama wake, mpaka atakapokata rufaa na kusikilizwa na Baraza Kuu la Chadema, lenye wajumbe kutoka kila pembe ya nchi.

Dk Slaa hivi karibuni alitamka kuwa Baraza litaitishwa wakati wowote na hawamwogopi Zitto, kauli ambayo haijatekelezwa kama iliyopata kutolewa na Lissu, kwamba Chadema itafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri Kivuli.

Lissu katika tamko lake mwanzoni mwa kikao kilichopita cha Bunge Novemba mwaka jana, aliahidi kuwa Chadema itafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Kivuli na kuondoa aliowaita mawaziri vivuli ‘mizigo’, ambao walitafsiriwa kuwa ni wabunge waliokuwa wakimwunga mkono Zitto.

Matokeo

Uchaguzi mdogo uliofanyika juzi, CCM iliibuka na ushindi katika kata za Segela, Mpwayungu na Mirijo mkoani Dodoma; Nduli, Ibumu na Ukumbi mkoani Iringa na Ubagwe mkoani Shinyanga.

Ushindi huo pia ulipatikana katika kata ya Magomeni na Kibindu mkoani Pwani, ambako pia Mbowe alifika na helikopta wakati wa kampeni na kata za Kiomoni na Mtae mkoani Tanga.

Mkoani Lindi CCM ilipata ushindi katika kata za Kiwalala na Namikago; pamoja na kata ya Mkwiti, Mtwara. Rukwa CCM ilishinda kata ya Kasanga huku Mbeya ikiibuka na ushindi katika kata za Malindo na Santilya na mkoani Mara, ikishinda katika kata ya Nyasura.

Morogoro, CCM iliibuka na ushindi katika kata za Tungi na Rudewa, huku mkoani Manyara ikishinda katika kata za Partimbo na Loolera. Mkoani Kigoma, CCM ilitwaa kata ya Mkongolo, ambayo awali ilikuwa ikiongozwa na Diwani wa Chadema na kata ya Kilelema, ilichukuliwa na NCCR-Mageuzi, ambayo imedhihirisha mkoa huo kuwa ngome yake.

Hata hivyo, mkoani Njombe, Chadema ilitwaa kata ya Njombe Mjini kutoka mikononi mwa CCM, huku ikidhihirisha umwamba kwa kuchukua kata ya Sombetini mkoani Arusha na kuendelea kuongoza kata ya Kiboroloni, Kilimanjaro ambako kuna ngome yake imara.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. New EAC Blog - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger